Jitihada za Serikali Katika Kupambana na Madawa ya Kulevya

Kete za madawa ya kulevya

Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.

TATIZO LA MADAWA YA KULEVYA bado limekuwa likiendelea kuwepo katika maeneo mengi nchini kwa kipindi cha mwezi Oktoba licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali kwa lengo la kupunguza matumizi na upatikanaji wa dawa hizo.

Baadhi ya matukio ya ukamataji wa dawa za kulevya pamoja na watuhumiwa wa dawa hizo yalitokea nchini katika kipindi hicho, hali ambayo inadhihirisha juu ya uwepo wa tatizo hilo katika kipindi hicho.

Taarifa toka Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Sehemu ya Elimu, Habari na Takwimu inaeleza kwamba, mnamo tarehe 23 Oktoba, mwaka huu zilikamatwa kilo 4.547 za dawa aina ya Heroin na gramu 894.28 za dawa aina ya Cocaine katika eneo la Magomeni, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo la ukamataji wa dawa hizo, jumla ya watuhumiwa watano ambao ni raia wa Tanzania waliohusishwa na dawa hizo walikamatwa, pia tarehe 30 Oktoba, 2014 zilikamatwa dawa nyingine kilo 41.7 za Heroin zikiingizwa nchini zikiwa zimewekwa katika Jahazi katika Bahari ya Hindi, ambapo katika tukio hilo raia wa Iran wapatao 13 walikamatwa na wanashikiwa na Jeshi la Polisi kwa kujihusishwa na biashara hiyo.

Aidha, tarehe 31 Oktoba mwaka huu katika eneo la Ununio wilayani Kinondoni nje ya Jiji la Dar es Salaam zilikamatwa kilo 35.2 za Heroin zikiwahusisha watuhumiwa wawili ambao ni raia wa Nigeria pamoja na Pakistan.

Katika tukio lingine la tarehe 24 Oktoba, 2014 alikamatwa mtanzania akiwa na gramu 0.85 za Heroin na gramu 1.72 za bangi vikiwemo na vifaa vinavyotumika kutumia dawa hizo, hivyo hali hii inaashiria kuwa matumizi ya dawa za kulevya bado ni tatizo nchini.

Pamoja na mapambano makali dhidi ya madawa ya kulevya, kumekuwapo na viashiria vingine vya uwepo wa biashara hiyo, kwani kumegundulika uwepo wa mashamba ya bangi katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

Katika kipindi hicho, mashamba ya bangi ambayo hulimwa kwenye mapori na miinuko mikali yaligunduliwa na kuharibiwa hapa nchini, ambapo siku ya tarehe 29 Oktoba, 2014 kufuatia operesheni iliyofanywa na Kikosi Kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, jumla ya ekari nne za mashamba ya bangi, magunia 267 ya bangi na gunia moja la mbegu yaliteketezwa katika vijiji vya Kisimiri Juu na Olkokoola wilayani Arumeru, mkoani Arusha.

Aidha, operesheni kama hiyo ilifanywa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro Vijijini ambapo zaidi ya ekari nne za mashamba ya bangi ziliteketezwa.
Suala la ukamataji wa dawa za kulevya umeendelea kuhusisha raia wa kitanzania pamoja na wale wa kigeni, hivyo hii inadhihirisha kwamba biashara hiyo ni uhalifu wa kimtandao ambao unahitaji ushirikiano wa wadau wa ndani na nje ya nchi katika kuudhibiti kwake.

Halikadhalika, Serikali imeendelea kushirikiana kwa karibu na nchi nyingine pamoja na Mashirika ya Kimataifa katika kudhibiti tatizo la dawa hizo ambapo matumizi ya dawa hizo yanadhirishwa na idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya waliojitokeza kupata matibabu katika vituo na hospitali mbalimbali vilivyopo nchini.

Taarifa inaeleza kuwa, mpaka mwisho wa mwezi Oktoba, jumla ya watumiaji wa dawa za kulevya aina ya heroin wapatao 1,805 wakiwemo wanawake 232 waliendelea kupatiwa tiba ya methadone katika Hospitali za Mwananyamala, Temeke pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Licha ya mafanikiop yaliyopatikana katika mwezi Oktoba, jitihada za kukabilina na tatizo la dawa za kulevya zitainmarishwa ikiwa ni pamoja na kuboresha Sheria za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya, kutoa elimu kwa umma, kuendesha operesheni za kukamata dawa za kuolevya pamoja na wafanayabiashara wa dawa hizo.

Matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya yana umuhimu katika jamii hapa nchini, na matibabu hayo yataendelea kutolewa ikiwa ni pamoja na kukabilina na unyanyapaa kwa watumiaji wa dawa za kulevya ili waweze kujitokeza kupata matibabu hayo.

Aidha, ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa udhibiti wa tatizo la dawa hizo unapaswa kuimarishwa zaidi na wananchi kwa namna moja wanapaswa na kuaswa kutoa taarifa sahihi zitakazoweza kusaidia kufichuliwa kwa uhalifu na kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa hizo.