RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Novemba 8, 2014, alifanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.
Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa Rais alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo. Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa. Hali ya Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba. Wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
Imetolewa na KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
DAR ES SALAAM, NOVEMBA 9, 2014