TGNP Mtandao imefuatilia kwa karibu taarifa mbalimbali za hivi karibuni kuhusu upungufu wa dawa na vitendea kazi katika taasisi za afya ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati humu nchini. Hali hii imetokana na Bohari ya Dawa (MSD) kusitisha utoaji wa dawa muhimu kwa taasisi za afya za serikali hadi hapo deni la shilingi bilioni 90 linalodaiwa na bohari hiyo litakapolipwa.
Taarifa zinaonesha kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inadaiwa kiasi hicho cha fedha ambacho ni gharama za uingizaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba mbalimbali. Kutolipwa kwa gharama hizo kumefifisha uendeshaji wa bohari ya dawa kiasi kwamba, katika kipindi kifupi kijacho haitoweza kuendesha shughuli zake.
Kushindwa kulipwa kwa deni hilo kunababisha upungufu wa dawa na vifaa tiba na kuchelewa kwa manunuzi na usambazaji miongoni mwa matatizo mengine. Tatizo hili linatokana na ufinyu wa bajeji ambapo serikali hijachukua hatua mahsusi na kuweka kipaumbele katika sekta ya afya ambapo katika bajeti ya mwaka 2014/15 manunuzi ya dawa yalitengewa kiasi cha shilling bilioni 77.5 chini ya mahitaji halisi ya shilingi bilioni 500.
Ikiwa ni matokeo, hali hii imesababisha kuzorota kwa utoaji wa huduma katika taasisi hizo na kusababisha usumbufu na madhara kwa wananchi wanaohitaji huduma. Taarifa zinaonesha kuwa hata hospitali ya Taifa Muhimbili inayodaiwa kiasi cha shilingi Bilion 8 imeathirika kwa kiwango kikubwa. Na sasa imelazimika kuongeza gharama za matibabu kutoka sh. 20,000 kwa siku zote anazotibiwa hadi sh. 5,000/= kwa kila siku na sh. 2,000/= za chakula kila siku ili kuwezesha kulipa deni hilo.
Tatizo hili linasikitisha kwani linaathiri zaidi Wanawake, watoto, wenye ulemavu na wazee ambao hawana rasilimali za kutosha na wanategemea huduma ambazo hupatikana katika taasisi za afya za serikali. Waathirika wengi wa hali hii ni wananchi wa kawaida ambao hawana uwezo wa kupata huduma katika taasisi binafsi za afya. Kadhalika, kutokama na kuwa, zaidi ya asilimia 80% ya watanzania hawana bima za afya itakayowawezesha kupata huduma za kiafya hatua madhubuti za dharura zichukuliwe ili kuokoa maisha ya wengi.
TGNP Mtandao tumekuwa tukidai kutengwa kwa bajeti ya kutosha inayokidhi azimio la Abuja la kutenga kiasi cha asilimia 15 ya fedha zetu za ndani kwa ajili ya bajeti ya afya.
Aidha tatizo tunaloliona ni kutokana na sekta ya afya kutokupewa kipaumbele kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15. Kutokana na kuendelea kutokuipa kipaumbele sekta ya afya, taarifa ya 14 ya Hali ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2013 iliyoandaliwa na shirika la Save the Children, imeiweka Tanzania katika nafasi ya 135 kati ya nchi 176 ambazo ni nchi hatari kwa wanawake kujifungua.
TGNP Mtandao, kama shiriki la kutetea haki za kijamii hasa kwa wanawake, watoto, walemavu na makundi mengine yaliyoko pembezoni, tunaamini kuwa watoto na wanawake ni wahanga wakubwa wa hali hii wakiwemo wanawake wajawazito ambao wengi katika baadhi ya hospitali za serikali hujifungulia katika mazingira hatarishi. Hivyo, TGNP Mtandao tunapendekeza yafuatayo;
– Serikali kupitia wizara husika kuchukua hatua za dharura ili kuepusha madhara zaidi kwa wananchi ambao wengi ni masikini.
– Serikali kutenga fedha za kutosha kwenye bajeti ya afya inayozingatia jinsia (Gender Budgeting) kila mwaka ili kukidhi mahitaji yake na kusimamia rasilimali fedha inayotolewa kikamilifu.
– Ni wakati mwafaka kwa serikali kuhakikisha kuwa bajeti ya sekta ya afya ya mwaka 2015/16 inaongezwa ili kuiwezesha bohari ya dawa kujiendesha kwa ufanisi
– Sekta ya afya ipewe kipaumbele kama zilivyo sekta nyingine katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ili ifikie 15% ya bajeti kama ilivyoagizwa katika azimio la Abuja.
– Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuacha mara moja kuwabebesha wananchi mzigo wa kulipia deni la MSD haraka badala yake serikali iwawajibishe waliozembea kuwezesha ulipwaji wake.
Imetolewa na; Lilian Liundi,
Kaimu Mkurugenzi TGNP Mtandao