Mambo Yaharibika Bukina faso Jeshi Lapindua Nchi

Jenerali Honore Traore

Jenerali Honore Traore

AMIRI Jeshi Mkuu wa Jeshi la Burkina Faso, Jenerali Honore Traore ametangaza kuvunjwa kwa serikali na bunge la nchi. Kiongozi huyo mkuu wa jeshi hata hivyo hakuweka wazi ni nani atakayeshikilia uongozi wa taifa hilo kwa sasa.

Jenerali Traore aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutaundwa serikali ya mpito baada ya kufanyika mazungumzo baina ya wanasiasa wa upinzani na kiongozi aliyepinduliwa Rais Blaise Campaore. Jenerali Traore alikuwa akiwahutubia waandishi wa habari baada ya kushuhudia kundi kubwa la maandamano katika Mji Mkuu wa Ouagadougou.

Waandamanaji walivamia majengo ya Bunge na majumba ya wafuasi wa Rais Blaise Compaore na kuyachoma wakipinga azimio lake la kutaka kubadilisha katiba ya taifa ilikumruhusu kuwania kipindi kingine cha uongozi baada ya kutawala kwa zaidi ya miaka 27.

Awali Waandamanaji waliteketeza majengo ya Bunge mjini Ougadougou na kuwatimua wabunge. Kituo cha Televisheni cha Taifa kililazimika kusitisha matangazo baada ya waandamanaji kuvamia shirika hilo la utangazaji la taifa.

Waandamanaji kisha wameelekea Ikulu ya Rais na wanajeshi wamekua wakiwafyatulia risasi. Vilevile baraza la jiji pamoja na makao makuu ya chama tawala yameteketezwa moto. Umati mkubwa wa watu umeonekana ukielekea ikulu ya Rais huku uwanja wa ndege ukifungwa. Wakati vurugu hizo zikiendelea Rais Blaise Compaore aliwaomba wananchi kutulia katika ujumbe alioutuwa kwa mtandao wa Twitter.

Wabunge wamelazimika kuahirisha kupiga kura hiyo ya kubadilisha katiba kumkubalia Compaore kuwania tena Urais mwaka ujao. Watu watano wameuawa katika maandamanao hayo ambayo yametajwa kuwa mabaya zaidi kukumba utawala wa Blaise Compaore. Awali wanajeshi waliwafyatulia risasi waandamanaji waliovamia majengo ya bunge.

Compaore alitwaa madaraka kupitia mapinduzi mwaka wa 1987. Amekua akishinda uchaguzi lakini kura hio hukumbwa na utata. Ufaransa na muungano wa Ulaya zimemuomba Rais Compaore kutobadilisha katiba ili kuwania tena.
-BBC