Rais TFF Kufungua Kozi ya Futuro III, Abubakar Mchezaji Bora

Kiungo Salum Abubakar kushoto akiwa kazini.

Kiungo Salum Abubakar kushoto akiwa kazini.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi Oktoba 29 mwaka huu anafungua kozi ya ukufunzi wa waamuzi ya FUTURO III ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Hafla ya ufunguzi wa kozi hiyo inayoshirikisha zaidi ya waamuzi 40 wakiwemo baadhi ya wale ambao bado wanachezesha mpira wa miguu kutoka nchi mbalimbali za Afrika itafanyika saa 4 asubuhi kwenye hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam.
 
Kati ya hao, washiriki wanane wa kozi hiyo inayoanza kesho hadi Novemba 3 mwaka huu chini ya wakufunzi wa FIFA wakiongozwa na Carlos Henriques ni kutoka Tanzania. Washiriki kutoka Tanzania ni Emmanuel Chaula, Joan Minja, Josephat Bulali, Paschal Chiganga, Ramadhan Ibada, Richard Kayenze, Samuel Mpenzu na Soud Abdi.
 
SALUM ABUBAKAR MCHEZAJI BORA OKTOBA
Kiungo wa timu ya Azam, Salum Abubakar amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini. Abubakar ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) aliwashinda wachezaji wengine 20, huku wanne kati ya hao wakichuana naye kwa karibu.
 
Wachezaji hao ni Joseph Mahundi wa Coastal Union, Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar) na Najim Magulu wa JKT Ruvu Stars. Kwa kuibuka mchezaji bora, Abubakar atazawadiwa kikombe na fedha taslimu sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
 
Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.