Ufaransa Yakubali Kuitangaza Zanzibar Kiutalii

Baadhi ya maeneo ya kitalii mjini Zanzibar

Baadhi ya maeneo ya kitalii mjini Zanzibar

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

UFARANSA imeahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini mwake kupitia makampuni yake makubwa ya kitalii yaliopo nchini humo sambamba na kuendelea kuziunga mkono sekta nyengine za maendeleo za hapa nchini.

Balozi mpya wa Ufaranza nchini Tanzania, Malika Berak aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwemyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Berak alimuhakikishia Dk. Shein kuwa afisi yake itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha Makampuni makubwa yanayofanya kazi za kitalii yaliopo nchini Ufaransa pia, yanafanya kazi zake na hapa Zanzibar.

Alisema kuwa kutokana na Ufaransa kupiga hatua kubwa katika sekta ya Utalii sambamba na kuwa na watalii wengi wanaotembelea nchi mbali mbali ikiwemo Zanzibar ni jambo la busara kwa makampuni hayo kuongeza juhudi na kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika sekta ya utalii

Balozi huyo wa Ufaransa alisema kuwa kwa vile Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii pamoja na mikakati madhubuti iliyowekwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo hivyo nchi hiyo nayo iko tayari kuziunga mkono juhudi hizo.

Aidha, Balozi Berak alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano wake na kuimarisha uhusiano uliopo kwa kushirikiana pamoja katika kuinua sekta mbali mbali za maendeleo na kiuchumi ikiwa ni pamoja na ushirikiano kwenye sekta ya elimu, utamaduni na nyenginezo.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimpongeza Balozi huyo mpya wa Ufaransa nchini Tanzania na kumueleza kuwa Zanzibar na Ufaransa zina uhusiano wa muda mrefu tokea karne ya 19.

Dk. Shein alisema kuwa azma hiyo ya Ufaransa ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuitangaza na kuiimarisha sekta ya utalii nchini mwake itasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi hasa ikizingatiwa kuwa Ufaransa ni miongoni mwa nchi ambayo watalii wake wengi huitembelea Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuimarisha sekta za maendeleo mikakati kabambe imewekwa na serikali anayoiongoza katika kuhakikisha huduma zote za kitalii zinaimarika ikiwa ni pamoja na uwekezaji na hali ya usalama katika sekta hiyo.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo wa Ufaransa kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo na kusisitiza kuwa ipo haja ya kuendelezwa kupitia sekta ya elimu kwa wanafunzi kutoka Ufaransa kuja kusoma kiswahili hapa Zanzibar na wale wa Zanzibar kwenda nchini humo kujifunza.

Akitoa historia ya uhusiano kati ya pande mbili hizo, Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kuweka Ubalozi wao mdogo hapa Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12,1964 ni Ufaransa ambapo alimueleza balozi huyo haja ya kuwepo huduma hizo kwa kuanzisha Ubalozi mdogo au huduma za Balozi wa heshima ili ubalozi huo uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pia, alifanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ali Said Siwa ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumuaga Rais na kutoa shukrani zake kwa Dk. Shein kwa kumpa moyo na kumuamini katika utendaji wake wa kazi.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alimpongeza Balozi huyo Mteule kwa kuteuliwa kuwa Balozi nchini Rwanda na kumueleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania ikiwemo Zanzibar na Rwanda na kumueleza haja ya kuimarishwa na kuendelezwa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Rwanda zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo elimu, utalii wa ndani huku akisisitiza haja kwa wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwa kuadhimisha siku ya taifa ya nchi hiyo.

Katika salamu zake hizo Dk. Shein amesema yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar wanayo furaha katika kuadhimisha siku hii ya Taifa ya nchi hiyo na kumpongeza Mheshimiwa Erdogan kwa kuiongoza vyema Uturuki sambamba na kuimarisha umoja na kuleta ustawi wa wananchi wake.