Waziri Mkuu Pinda ‘Alilia’ Wawekezaji Poland

Jiji la Warsaw nchini Poland

Jiji la Warsaw nchini Poland


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewasili nchini Poland kwa ziara ya siku mbili ya Kiserikali ambayo inalenga kuwavutia wafanyabiashara wa nchi hii waje kuwekeza Tanzania. Mara baada ya kuwasili jijini Warsaw, akitokea London Uingereza, Waziri Mkuu Oktoba 23, 2014 alikutana na wafanyabiashara zaidi ya 50 kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za Chama cha Wafanyabiashara cha Poland (Polish Chamber of Commerce).
 
Katika Mkutano huo, Waziri Mkuu aliwaeleza mipango ya Serikali ya kuikwamua Tanzania kiuchumi huku akigusia sekta za kilimo, uvuvi, uchukuzi, miundombinu, madini, nishati na utalii.
 
“Nia ya ziara yangu fupi lakini yenye malengo mahsusi ni kuamsha mahusiano baina ya nchi zetu mbili lakini zaidi ni kutafuta mbinu za kukuza biashara kati ya Tanzania na Poland. Nataka muione Tanzania kama mahali salama pa kuwekeza mitaji yenu, mahali rafiki pa kuweka mitaji lakini pia mahali pa kufanya biashara ambayo pia itahusisha uwekezaji,” alisema.
 
Katika mkutano huo Waziri Mkuu alijibu maswali kutoka kwa wafanyabiashara zaidi ya 10 ambao walikuwa na shauku ya kutaka kufahamu ni maeneo yapi zaidi yanayohitaji uwekezaji. Pia aliishukuru Serikali ya Poland kwa kusaidia ukarabati na uimarishaji wa miundombinu kwenye Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru, kilichopo Arusha.
 
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuongea na wafanyabiashara hao, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati, Bibi Katarzyna Kacperczyk alisema nchi hiyo imeanzisha mpango maalum ujulikanao kama “Go Africa” ambao umelenga kukuza mahusiano ya kiuchumi na bara la Afrika.
 
“Tukiwa ndani ya Jumuiya ya Ulaya, pamoja na hatua kubwa za kiuchumi tunazokwenda nazo, kama Serikali tuliamua kwa dhati kwamba hatuwezi kuwaacha ndugu wetu wa iliyokuwa Ulaya Mashariki kabla ya mageuzi ya kiuchumi duniani…lakini tumeamua kuangalia bara la Afrika kama mdau muhimu wa maendeleo lakini pia kama soko la uhakika kwa bidhaa tunazozalisha,” alisema.
 
Alisema mpango huo umeanzisha mahsusi ili kuwasaidia wafantabiashara wa Poland kupata taarifa sahihi na haraka kuhusiana na masuala ya ushirikiano na uwekezaji barani humo. Alisema wameanzisha mpango huo ili kuwahamasisha wenye makampuni barani Afrika waone kuna wenzao wa Poland na waamue kushirikiana katika kulijenga bara la Afrika.
 
Waziri Mkuu leo atatembelea kampuni ya Rol Brat inayotengeza zana za kisasa za kilimo yakiwemo matrekta na mashine za kuvuna mazao mazao mashambani. Pia atatembelea kampuni ya “Mtynpol” ambayo inahusika na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia vyakula na miundombinu yake. Kesho asubuhi atakutana na Watanzania waishio Poland na baadaye kufanya vikao na baadhi ya wafanyabiashara wa jijini Warsaw.