RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika katika Jamhuri ya Watu wa China kuendelea kutangaza habari njema kuwa bado ni salama kutembelea Bara la Afrika pamoja na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola ambao umeua maelfu ya watu hasa katika nchi tatu za Afrika Magharibi.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania imetuma madaktari watano kwenda Afrika Magharibi kusaidia kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao unaendelea kuua maelfu ya watu katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone. Mpaka sasa watu zaidi ya 4,000 wamepoteza maisha kwa ugonjwa huo katika nchi hizo.
Rais Kikwete pia amesema kuwa ni muhimu zaidi kwa nchi za Afrika kuongeza mshikamano na kusaidiana, ili kuongeza nguvu za pamoja za kukabiliana na ugonjwa huo ambao umeanza kuwa tishio kwa dunia nzima. Rais Kikwete ameyasema hayo, Oktoba 22, 2014, kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni ya Serikali ya Diaoyutai mjini Benjing, wakati alipokutana na kuzungumza na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao nchini China ikiwa ni shughuli yake ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali nchini humo.
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete aliwasili mjini Beijing, usiku wa jana, Jumanne, Oktoba 21, 2014, kuanza ziara rasmi ya siku sita katika China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping. Katika mkutano wake na mabalozi hao wa Afrika, Rais Kikwete amepata nafasi ya kuwaeleza hali ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama Barani Afrika hasa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Libya, Sudan Kusini na Somalia na tishio la ugaidi wa makundi mbali mbali katika nchi za Afrika.
“Lakini habari kubwa katika Afrika kwa sasa ni ugonjwa wa Ebola. Bara la Afrika linabaguliwa sasa kwa sababu ya ugonjwa huo. Watu wanafuta mipango yao kutembelea Bara letu, watalii wanapungua. Kwetu sisi ugonjwa huu ni tishio kubwa kwa maisha ya watu wetu lakini ni tishio kubwa kiuchumi,” Rais Kikwete amewaambia mabalozi hao na kuongeza:
“Sasa kwa sababu ugonjwa wa Ebola unaongeza kubaguliwa kwa Bara la Afrika, ni wajibu wenu nyie wawakilishi wetu, mabalozi wetu kutusemea. Elezeni habari njema na nzuri za Afrika. Waambie hawa wakubwa kuwa Bara la Afrika ni Bara salama kutembelea pamoja na kushambuliwa na ugonjwa wa Ebola. Aidha, kwa sababu kuna majaribio ya dawa nyingi za ugonjwa huo yanafanyika katika nchi mbali mbali ikiwemo China, waombe wakubwa hawa watusaidiE kupatikana kwa dawa hizo.”
Kuhusu mchango wa Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania imetuma madaktari wake watano katika nchi zinazokabiliwa na ugonjwa huo kwa sasa kuongeza nguvu za kukabiliana na Ebola. “Nchi za Afrika zinahitaji sana mshikamano na ushirikiano kwa sasa kukabiliana na ugonjwa huo hatari sana.”