TPB Yawapa Somo la Akiba Wanafunzi Sekondari ya Jangwani
WAZAZI na walenzi wametakiwa kuwa na mazoea ya kuwawekea watoto wao akiba ili iweze kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo elimu.
Mwito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Nchini (TPB) Sabasaba Moshingi, wakati wa semina iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani.
Alisema, katika kuadhimisha miaka 90 ya siku ya kuweka akiba duniani inayofanyika kila Oktoba 30 benki yao iliazimia kutembelea taasisi mbalimbali zikiwemo shule za sekondari ili kuwafahamisha umuhimu wa kuweka akiba.
Alisema, katika takwimu zilizofanywa na watu mbalimbali zinaonesha kuwa asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia huduma za kibenki, huku asilimia tatu wakiwa wanatumia huduma ya mikopo.
“Kwa hapa nchini uwekaji akiba ni asilimia 10 ambao upo chini ya GDP, huku nchi za Afika uwekaji akiba ukiwa chini sana ikilinganishwa na Bara la Asia ambalo uwekezaji wake ni mara nne zaidi ya nchi za Afrika,” alisema Moshingi.
Alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni watu wengi kutokuwa na elimu juu ya umuhimu wa kuweka akiba ili ziweze kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye.
“Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa watu wengi wenye mafanikio makubwa katika nchi mbalimbali walifanikiwa kwa kuweka akiba, hivyo ni wajibu wetu sisi kama wazazi na walezi kuwawekea watoto wetu akiba zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Moshingi.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Jangwani, Geradin Mwanisenga, alisema semina hiyo ni fursa nzuri kwa walimu na wanafunzi wa shule yake kwani wengi wao hawafahamu umuhimu wa kujiwekea akiba.