Rais Kikwete amuaga Rais wa Somalia

Rais wa Jamhuri ya Somalia, Mheshimiwa Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, ameondoka nchini leo, Jumatano, Agosti 10, 2011 mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili ya kikazi katika Tanzania.

 Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kiongozi huyo wa Somalia ameagwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na viongozi wengine wa Serikali wakiwamo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Ndege iliyombeba Rais Sheikh Ahmed na ujumbe wake iliondoka uwanja wa ndege kiasi cha saa 4:30 asubuhi.

 Ujumbe huo wa Jamhuri ya Somalia uliwasili nchini asubuhi ya jana, Jumanne, Agosti 9, 2011 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Kikwete.

 Wakati wa ziara yake, Rais Sheikh Ahmed na ujumbe wake ulifanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Serikali ya Jamhuri ya Somalia na ile ya Tanzania, na baadaye jioni Rais Kikwete alimwandalia mgeni wake futari ambayo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwamo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao za  nje katika Tanzania.

 Wakati wa mazungumzo rasmi na baadaye wakati wa futari, Rais Kikwete alitangaza kuwa Tanzania itatoa kiasi cha tani 300 za mahindi kwa ajili ya kusaidia wahanga wa ukosefu mkubwa wa chakula katika Somalia. Kiasi cha wananchi milioni 3.5 wa Somalia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

 Rais Kikwete pia amesema kuwa nchi hizo mbili zimekubaliana kufanya jitihada za pamoja kukabiliana na changamoto za pamoja zinazozikabili nchi hizo mbili ukiwamo uharamia katika Bahari ya Hindi ambao chanzo na asili yake ni Somalia.

 Imetolewa na:

 Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

10 Agosti, 2011