Beki ya Posta Yasaidia Vifaa vya Usafi Soko la Samaki Feri

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta (TPB), Sosthenes Nyenyembe akikabidhi kifaa cha kuhifadhia uchafu (dustbin) kwa Meneja wa Masoko Halmashauri ya Ilala Athuman H. Mbelwa, katikati akishuhudia tukio hilo ni Meneja wa Soko la Samaki Feri Mkuu B. Hanje.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta (TPB), Sosthenes Nyenyembe akikabidhi kifaa cha kuhifadhia uchafu (dustbin) kwa Meneja wa Masoko Halmashauri ya Ilala Athuman H. Mbelwa, katikati akishuhudia tukio hilo ni Meneja wa Soko la Samaki Feri Mkuu B. Hanje.

BENKI ya Posta imekabidhi msaada wa vifaa vya usafi vyenye thamani ya shilingi milioni 4 kwa uongozi wa soko Kuu la Samaki la Feri. Msaada huo umetolewa baada ya uongozi wa soko la Feri kupeleka maombi kwa uongozi wa benki hiyo kuomba kusaidiwa vifaa vya kufanya usafi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa Benki ya Posta, Sosthenes Nyenyembe alisema kuwa vifaa walivyonunua ni pamoja na mapipa ya kuhifadhia taka, makoleo, mafagio na matoroli.

Alisema, soko hilo kwa siku linaingiza watu zaidi ya 7,000 kutoka sehemu mbalimbali wakiwemo watalii wanaokuja kwa ajili ya shughuli tofauti nchini. “Tukiwa kama wadau wa maendeleo na mazingira ni wajibu wetu kuhakikisha tunaboresha usafi wa soko hili na kuliweka katika hali ya usafi ili kuwakinga na magonjwa ya mlipuko wafanyakazi na wanunuzi wa soko hili,” alisema Nyenyembe.
 
Aidha alisema kuwa wataendelea na utaratibu wa kusaidia masuala ya maendeleo ikiwa ni njia mojawapo ya kurejesha faida wanayoipata kutoka kwa wateja wao.
 
Kwa upande wake Ofisa Masoko wa Manispaa ya Ilala, Athumani Mbelwa aliupongeza uongozi wa benki hiyo kwa msaada waliowapatia na kutaka taasisi nyingine kuiga mfano huo. Alisema kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ukusanyaji wa taka zinatotokana na samaki katika soko na kuondoa mrundikano wa taka pindi gari linapokosekana.
 
“Soko letu huwa katika mazingira mabaya pale gari la kubeba taka linapokosekana hivyo vifaa hivi vitatusaidia kuhifadhia taka na kuliweka soko hili katika hali ya usafi muda wote.” alisema Mbelwa.