Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jana, Jumanne, Agosti 9, 2011, amempokea mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Somalia, Mheshimiwa Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Kikwete.
Ndege iliyomleta Rais wa Somalia, iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mjini Dar es Salaam saa tano kamili asubuhi na baada ya shughuli za protokali ya mapokezi, Rais Kikwete amemwacha mgeni wake kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency ambako alifikia wakati wa ziara hiyo.
Viongozi hao wawili wataongoza mazungumzo rasmi kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Somalia kabla ya Rais Kikwete kumwalika Mheshimiwa Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kwenye futari jioni. Matukio yote mawili yatafanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Kiongozi huyo wa Somalia na ujumbe wake ambao ni pamoja na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Somalia, Mheshimiwa Aidid Abdullahi Ilka Hanaf na Naibu Mawaziri Wakuu Mheshimiwa Hussein Arab Isse na Mheshimiwa Mohammed Mohamud Ibrahim, wataondoka nchini Jumatano, Agosti 10, 2011.