Maonesho ya Jua Kali Kufanyika Kigali

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdalah Kigoda.

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Dk. Abdalah Kigoda.

Na James Gashumba, EANA

MAONESHO ya kanda maarufu kwa jina la Jua Kali/Nguvu Kazi yatafanyika mjini Kigali, Rwanda Desemba 1, mwaka huu. Maonesha hayo yanayoandaliwa chini ya kauli mbiu “Kuendeleza uchumi mdogo na Sekta Endelevu ya Ujasiliamali kwa Mtangamano na Kukuza Uchumi,” yanatarajiwa kuhudhuriwa na wabunifu wapatao 1,000 kwa mujibu wa serikali ya Rwanda.

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Rwanda, Francois Kanimba alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kigali kwamba tukio hilo la kila mwaka litatoa nafasi kwa wajasiliamali wenyeji kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Tunafanyakazi kwa karibu na nchi wanachama kuhakikishwa kwamba maonyesho hayo yanatambulika zaidi na uwekezaji unaelekezwa kwenye sekta isiyorasmi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi. Kuendeleza biashara ndogondogo ni suala muhimu katika mtangamano wa kiuchumi,” alisema Waziri Kanimba.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kufanyakazi na wadau wote kuiunga mkono sekta hiyo kupitia utoaji tuzo kama vile ya Mpango wa Zawadi ya Kazi Bora ya Mikono. Washiriki wa maonesho hayo watakuwa na fursa za kuonyesha bidhaa zao kutoka kanda hiyo ya EAC na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu katika masuala mbalimbali muhimu na ya msingi, kwa mujihu wa Kanimba.

Akizungumza katika mkutano huo wa waandishi wa habari pia, Mkurugenzi Mkuu wa Biashara na Forodha wa EAC, Peter Kiguta alizitaka nchi wanachama kuwekeza zaidi katika ubunifu, kuwajengea uwezo watu wao na kuziongezea thamani bidhaa zinazozalishwa ili kushindana katika soko la kanda.