Vituo 33 vya Kuwawezesha Vijana Kiuchumi Vyafunguliwa

Baadhi ya Vijana wa DSW wakifuatilia mada wakati wa mdahalo wa vijana kuhusu Stadi za Maisha ikiwa ni moja ya programu katika kuadhimisha Wiki ya Vijana ambayo kitaifa inafanyika mkoani Tabora. Picha na Frank Shija, Tabora.

Baadhi ya Vijana wa DSW wakifuatilia mada wakati wa mdahalo wa vijana kuhusu Stadi za Maisha ikiwa ni moja ya programu katika kuadhimisha Wiki ya Vijana ambayo kitaifa inafanyika mkoani Tabora. Picha na Frank Shija, Tabora.

Vijana wa DSW wakifafanua kuhusu progamu ya Kijana Kwa Kijana inayoendeshwa na Shirika lao kwa kushirikisha vikundi vya vijana. Picha na Frank Shija, Tabora.

Vijana wa DSW wakifafanua kuhusu progamu ya Kijana Kwa Kijana inayoendeshwa na Shirika lao kwa kushirikisha vikundi vya vijana. Picha na Frank Shija, Tabora.


SHIRIKALISILO la Kiserikali linalojihusisha na changamoto zitokanazo na ongezeko la idadi ya watu, DSW limefungua jumla ya vituo 33 kote nchini kwa ajili ya kuwaelimisha vijana kuhusu masuala ya afya na uzazi, kujitambua na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mjini Tabora, Meneja Mkazi wa Miradi washirika la DSW nchini Tanzania, Avit Buchwa alisema vituo hivyo vimefunguliwa kwa ajili ya kuwaelimisha vijana kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili wabadilike na kuibadilisha jamii. Vituo hivyo ni sehemu muhimu kwa vijana kwani wanaweza kutoa mawazo yao kwa uwazi kwa jamii inayowazunguka.

Bw. Buchwa ametaja mikoa ambayo shirika hilo limefungua vituo kuwa ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara na Manyara. Katika mikoa hiyo vituo hivyo vinawafanya vijana kuwa karibu na jamii husika ambayo inakuwa rahisi kuonana kutambua changamoto zao na kuzishughulikia kikamilifu.

“Vijana wanapata fursa ya kuelimishwa kupitia Vituo vyetu vilivyoko katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kwasasa tumejikita zaidi katika kuelimisha Vijana kujitambua na kutatua changamoto zinazowakabili kupitia njia ijulikanayo kama kijana kwa Kijana Project,” alisema Buchwa.

Alisema kuwa katika vituo hivyo mtazamo rafiki kuhusu masuala ya afya ya uzazi kwa vijana unatumika katika shughulizao. Hii imesaidia katika kuvifanya vituo hivyo kuwa na ufanisi mkubwa katika utendaji wa kilasiku.

DSW linawawezesha vijana kujitambua na kufanya maamuzi sahihi, kuwajengea uwezo kiuchumi kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo ya maendeleo, kuwafundisha vijana stadi za kazi ikiwemo masuala ya uongozi na kuwaandalia ziara za kimafunzo ndani na nje ya nchi ili kuwapatia uzoefu mbalimbali, alisema Buchwa.

Aidha Buchwa alitoa rai kwa Serikali kupitia Halmashauri zote nchini kutoa kipaumbele masuala ya Afya ya Uzazi kwa Vijana yanaingizwa katika mipango ya (CCHP) na kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji ambapo alisema kwa kufanya hivyo kutatimiza haki ya msingi ya Kijana kupata mahitaji ya Kiafya.

Kwa upande mwingine, Katibu wa Kituo cha Vijana Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Aziz Salim alisema DSW imewasaidia sana vijana kupata mafunzo mbalimbali kuhusu stadi za maisha pia na kupatiwa pesa na mbegu kwa ajili ya miradi ya vijana. Ameongeza kuwa vijana makini ambao wamepata fursa ya kupata huduma katika Vituo vya Vijana (YEC) vinavyoendeshwa na DSW wamefanikiwa sana kubadilika kimaisha na kuwa na mtazamo chanya wa kimaendeleo.