OFISA Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura Oktoba 11, 2014 amezinduwa Bonanza la Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) lililofanyika viwanja vya Chuo Kikuu (UDSM) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hotuba yake, iliyosomwa kwa niaba na Ofisa Mkuu wa Biashara wa TTCL, Kanda ya Dar es Salaam, Karim Bablia aliwataka washiriki wa bonanza kutumia nafasi hiyo ya kuwa pamoja ili kufahamiana zaidi, kubadilishana mawazo na kushirikiana.
“…Bonanza hili limetuwezesha sisi Wanamichezo Wafanyakazi kuweza kufahamiana miongoni mwetu, kubadilishana mawazo ya nini kinafanyika kwenye kampuni, mashirika au taasisi zetu ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa za huduma na bidhaa tunazotoa kwa wateja wetu na wananchi kwa ujumla,” alisema Dk. Kazaura.
Aidha aliipongeza Kamati ya maandalizi ya bonanza hilo kwa kitendo cha kuwakutanisha pamoja wanamichezo hao, kwani mbali na kushindana kimichezo na kufahamiana wanapata fursa ya kujenga afya za wafanyakazi, umoja na undugu.
Alizishauri taasisi hizo kutenge muda maalum wa kufanya mazoezi kwenye taasisi zao kila siku kwa lengo la kuimarisha afya na kuiwezesha miili kuwa na nguvu ili kuzalisha tija zaidi kwenye sehemu zao za kazi, kwani taasisi kuwa na mfanyakazi lege lege haiwezi kuzalisha tija zaidi mahali pa kazi.
“…Napenda nitumie nafasi hii kuwapongezeni Kamati nzima ya Utendaji ya SHIMMUTA kwa jambo hili kubwa mlilofanya ambalo kusema kweli limetukutanisha sisi wanamichezo wafanyakazi mahala pamoja na kuweza kufanya michezo mbalimbali ambayo kwa hakika, naona imewawezesha
Wanamichezo Wafanyakazi wa rika zote kucheza kila mmoja na mchezo aliouzoea.
Hata hivyo alizipongeza taasisi na mashirika yaliyoshiriki katika bonanza hilo ikiwemo kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Chuo cha Tiba Muhimbili,(MUHAS) Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Taasisi ya Mifupa (MOI) Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Taasisi nyingine zilizoshiriki bonanza hilo ni pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Pamoja na hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu huyo wa Kampuni ya TTCL aliishauri SHIMMUTA kufikiria kuanzisha mabonanza kama hayo mikoa mingine ili kuhamasisha michezo kwenye mikoa hiyo na kujenga mahusiano mema miongoni mwa Wafanyakazi wa nchi hii. Mashindano yenyewe ya SHIMMUTA kwa mwaka 2014 yanatarajia kufanyika Mkoa wa Tanga kuanzia Novemba 20, 2014, ambapo itashirikisha michezo mbalimbali.