HATUA hiyo ya Dk Shein imekuja ikiwa ni wiki moja tangu mwanasheria huyo kukataa ibara 22 za Katiba inayopendekezwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma. Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Dk Abdulhamid Yahya Mzee imesema Rais Shein amempandisha cheo aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu, Said Hassan Said kuwa AG.
“Amefanya mabadiliko hayo kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Ibara ya 55(1), 53, 54(1) na 55(3)… Rais Shein ametumia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011, Kifungu cha 12(3) na 27,” ilisema taarifa hiyo.
Othman ambaye hivi karibuni alijiondoa katika Kamati ya Uandishi ya lililokuwa Bunge Maalumu kwa kutoridhika na baadhi ya mambo, alieleza bungeni kutokubaliana na ibara ya pili, tisa, 86, 37, 70 hadi 75 na Sura ya 11 ambayo ina ibara ya 158 hadi 161, Sura ya 16 yenye ibara za 243 hadi 251 na Nyongeza ya Kwanza inayozungumzia mambo ya Muungano.
Hatua hiyo ilionekana kuwaudhi baadhi ya wajumbe ambao walimzomea na baada ya Bunge kuahirishwa, alitolewa kupitia mlango wa nyuma wa Ukumbi wa Bunge chini ya ulinzi mkali.
Baadaye Othman aliliambia gazeti hili kwamba licha ya kuwa yeye ni Mwanasheria Mkuu wa SMZ, alitumia utashi wake wa kidemokrasia kupiga kura kuzikataa ibara hizo, kutokana na kutoridhishwa na jinsi zilivyoandikwa.
“Katika suala la Katiba, Serikali ilishatamka kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kwamba haina msimamo. Ndiyo maana uliona misimamo ilikuwa imeachwa kwenye vyama vya siasa, mimi siyo Mwanasheria Mkuu wa chama chochote.
“Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa maana ya upande… nilipiga kura kwa kuzingatia utashi wangu na maoni yangu.”
Ibara alizozikataa
Ibara ya 2. Hii inazungumzia eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likiwamo la Tanzania Bara na la Zanzibar pamoja na madaraka ya rais wa Jamhuri kugawa eneo lolote la nchi katika mikoa. Ibara ya 9 inayoeleza ukuu wa Katiba yenyewe na kuwa ndiyo sheria kuu. Inazuia kutungwa kwa sheria yoyote inayotofautiana nayo na inaelekeza wananchi na taasisi zote kuitii.
Sura ya Saba (Ibara 70-75). Hizi zinahusu muundo wa muungano na mgawanyo wa majukumu na mamlaka ya Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ. Pia ibara hizo zinafafanua wajibu wa viongozi wakuu katika kuhakikisha kuwa wanatetea, wanalinda, wanaimarisha na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara ya 86 na 87 inayofafanua utaratibu wa uchaguzi wa rais wa Muungano na taratibu za kisheria kwa mgombea asiyeridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu kupinga uchaguzi huo mahakamani.
Ibara ya 128. Hii inahusu mamlaka ya Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi katika kutunga sheria na kuzuia Baraza la Wawakilishi kutunga sheria juu ya jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge na kulizuia Bunge kutunga sheria kuhusu jambo lililoko chini ya Baraza la Wawakilishi.
Ibara za 159, 160, 161 zinazozungumzia Rais wa Zanzibar na majukumu yake, Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na majukumu yake.
Sura ya 16 (243-251). Hizo zinahusu Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano. Misingi ya matumizi ya fedha za umma, misingi inayoongoza matumizi ya fedha za Muungano, akaunti ya fedha ya pamoja, mfuko wa hazina na masharti ya kutoa fedha za matumizi katika mfuko huo.
Pia sura hiyo inaweka utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha kabla ya sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali, mfuko wa matumizi ya dharura na ulipaji wa mishahara ya baadhi ya watumishi. Nyongeza ya Kwanza. Hii ni orodha ya mambo ya Muungano ambayo yameongezwa kutoka saba ya Rasimu ya Warioba kuwa 14.
CHANZO: Mwananchi