SIDO IRINGA KUTOA MAFUNZO YA USINDIKAJI

Meneja Mkuu wa Shirika SIDO Iringa, Gervase Kashebo

Na William Macha, Iringa

SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda nchini (SIDO) mkoni Iringa linatarajia kutoa mafunzo ya usindikaji bora bidhaa za chakula hivi karibuni. Akizungumza ofisini kwake meneja mkuu wa shirika hilo mkoani hapa, Gervase Kashebo amesema mafunzo hayo ya usindikaji wa mchuzi, nyanya mvinyo pamoja na bidhaa nyingine zitokanazo na matunda ya msimu yatawalenga wajasiriamali kutoka mkoani Iringa.
Aidha ameongeza kuwa katika mafunzo hayo wajasiriamali watapatiwa mafunzo bora ya usindindikaji wa bidhaa zitokanazo na matunda pia wataejengewa uwezo mkubwa kwenye usindikaji wa vyakula kwa njia zinazokubalika kitaifa na kimataifa.
Pia watapewa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa biashara, uhimili wa masoko, ushindani, utunzaji kumbukumbu, pamoja na utafutaji wa masoko. Kashebo amesema, mafunzo hayo yanatarajiwa kuendeshwa na mtaalamu wa masuala ya usindikaji wa bidhaa hizo kutoka katika ofisi ya SIDO mkoa kwa kipindi cha wiki moja.
Katika hatua nyingine Kashebo amesema kwa kushirikiana na Mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini ( MUVI) wakulima wa nyanya watakuwa na uhakika na soko la zao hilo kwa kuwa mradi huo wa MUVI ambao pia upo chini ya SIDO umekuwa mstari wa mbele katika kusimamia vyema uzalishaji wa nyanya na alizeti mkoani hapa.
Mafunzo hayo yatawahusisha wajasiriamali 30 watakaojiandikisha na kuchangia gharama za mafunzo huku sehemu ya mafunzo hayo ikigharamiwa na SIDO. Kasebo amesema mwitikio ni mzuri kwani mpaka sasa wajasiriamali wapatao 20 wamejiandikisha kushiriki mafunzo hayo yatakayoanza Agosti 15, 2011.