RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, kuomboleza kifo cha Meja Jenerali Muhidin Kimario, Waziri Mwandamizi wa Zamani wa Serikali na Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF).
Aidha, Rais Kikwete amewatumia pole nyingi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange na familia ya Meja Jenerali Kimario kufuatia kifo hicho kilichotokea mchana, Oktoba 6, 2014, nchini India, ambako alikuwa anapata matibabu.
Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo kwa Waziri Mwinyi: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Meja Jenerali Muhidin Kimario, ambaye alilitumikia Jeshi letu kwa heshima kubwa na weledi wa kuigwa na baadaye kulitumikia Taifa letu kwa uaminifu na uadilifu wa kujivunia katika nafasi ya uwaziri.”
Ameongeza Rais Kikwete katika rambirambi zake: “Uhodari na ujasiri ule ule ambao Meja Jenerali Kimario aliuonyesha akiwa askari na ofisa mkuu ndio ule ule uliomwongoza katika utumishi wa umma na kwa nafasi zote za waziri mwandamizi, ambazo alizishikilia katika maisha yake iwe ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mkuu wa Mkoa ama Mkurugenzi wa Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA). Daima tutakosa uongozi na ushauri wake.”
“Nakutumia wewe Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki. Aidha, kupitia kwako, namtumia pole nyingi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na Jeshi letu lote kwa kuondokewa na ofisa mwenzao, kiongozi wao na mpiganaji mwenzao,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Aidha, kupitia kwako, natuma salamu zenye huzuni nyingi kwa familia ya Meja Jenerali Muhidin Kimario. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa wa kuondokewa na mhimili wa familia. Vile vile wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya Marehemu. Amin.”