Rais wa TFF Atoa Ufafanuzi Mvutano wa Kamati yake na Bodi
VYOMBO kadhaa vya habari vimeripoti kuhusu hali ya mgongano kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF na Bodi ya ligi Tanzania (Tanzania Premier league Board).
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania linapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1.Bodi ya ligi imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF kifungu 40(11). Hivyo Bodi ya ligi ni zao la Mkutano Mkuu wa TFF.
2.Katiba ya TFF imeipa mamlaka kamati ya utendaji ya TFF kutunga kanuni za uendeshaji wa Bodi ya ligi,kanuni hizi ndiyo nguzo kuu ya uendeshaji wa shughuli za Bodi ya ligi na ndizo zinaipa Bodi uhalali wake wa kuendesha shughuli zake za kila siku.
3.Bodi ya ligi ni chombo cha TFF kama vilivyo vyombo vingine vikiwemo kamati mbali mbali za TFF.Kisheria Bodi ya ligi sio chombo huru (its not a legal entity) hivyo Bodi pamoja na mambo mengine haina mamlaka ya kuingia mikataba ya aina yoyote ya kisheria .
4.Katiba ya TFF inatamka kuwa Bodi ya ligi itaheshimu na kufuata maagizo ya TFF.Maagizo haya yanatolewa na Sekretarieti ya TFF kwa niaba ya kamati ya utendaji ya TFF.
5.Mwenye mamlaka ya kutengua maamuzi ya kamati ya utendaji ya TFF ni Mkutano Mkuu wa TFF peke yake,hakuna chombo kingine cha chini chenye mamlaka hayo.
6.Kanuni za mashindano zinaandaliwa na kamati ya mashindano ya TFF na kupitishwa na kamati ya utendaji ya TFF. Kikao cha kamati ya utendaji kilichopitisha rasimu ya kanuni za ligi za mwaka 2014/15 kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa bodi ya ligi,Makamu mwenyekiti wa Bodi ya ligi na pia Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya TFF,hawa wote ni wajumbe wa Bodi ya ligi na walishiriki kikamilifu katika kikao cha kamati ya utendaji kilichopitisha kanuni za ligi 2014/15 ukiwemo na utaratibu wa mgawanyo wa mapato ya milangoni na ya udhamini.Katiba ya TFF inaagiza hivyo kuwa Viongozi wakuu wa Bodi ya ligi watakuwa pia ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF. Aidha mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi alikuwepo kwenye kikao hiki cha kamati ya utendaji kama mwajiriwa.
7. Uamuzi wa kuunda mfuko maalum wa kuendeleza soka la vijana ni uamuzi uliopitishwa na kamati ya utendaji.Lengo la kuanzishwa mfuko huu ni kuwa na chombo maalum ambacho kitakuwa kinakusanya fedha toka vyanzo mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.Kwa sasa miradi hii ni:
(a) Kuanzisha vituo vya kulea na kuendeleza vipaji vya watoto kuanzia miaka 8-17 (sports centres) katika kila mkoa nchini mwetu.Mradi huu ni mkubwa utahitaji nyenzo hasa walimu na vifaa.
(b) Kuandaa timu ya taifa umri chini ya miaka 12 kwa ajili ya mashindano ya Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Timu hii itaanza kuandaliwa mwaka huu Desemba baada ya mashindano ya kitaifa umri chini ya miaka 12. Hii timu itakusanywa na kuwekwa katika shule moja ya bweni ambapo watalelewa na kuendelezwa vipaji vyao wakiwa pamoja huku wanasoma.Tanzania tumeomba kuwa wenyeji wa fainali hizi.
(c) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 14 kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2017.
(d) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 17 kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 mwaka 2017.
(e) Kuandaa mashindano ya Taifa ya mpira wa wanawake na ligi ya taifa ya mpira wa wanawake.
Miradi yote hii muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania haina udhamini lakini ni lazima ifanyike ili tujihakikishie tunainua mpira nchini mwetu. Mafanikio ya miradi hii sio tu yatafaidisha na kuimarisha timu zetu za Taifa lakini pia yatakuwa chimbuko madhubuti la wachezaji mahiri wa vilabu vyetu vya mpira wa miguu.
Kimsingi tunatarajia kuwa vyanzo vikuu vya mapato ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya mpira Tanzania vitakuwa:
– Mapato yatokanayo na mechi za ligi zetu madaraja yote
– Mapato yatokanayo na mechi za kimataifa
– Wadhamini
– Serikali kuu kupitia bajeti za Wizara zenye dhamana ya michezo,halmashauri na vyuo
– Wafadhili
– Shughuli mbali mbali za kutunisha mfuko.
Kamati ya utendaji ya TFF ilimteua Bwana Leodeger Tenga kuwa mwenyekiti wa kwanza wa mfuko huu na wajumbe wake ni Bw Tarimba Abbas, Bw Ephraim Mafuru, Mzee Ayoub Chamshama Bw Frederick Mwakalebela na Mh Zarina Madabida. Bw Henry Tandau na Bw Boniface Wambura ni waratibu wa mfuko huu. Imani ya TFF ni kuwa wajumbe hawa kwa kutumia uzoefu wao katika uongozi wa jamii watatusaidia kuhakikisha mfuko huu unaanza vyema shughuli zake.
Upande wa TFF tumefungua akaunti maalum benki kwa ajili ya kuingiza fedha zote zinazokusanywa kama mchango wa TFF kwenye mfuko huu zikiwemo asilimia 5 za makato ya fedha za udhamini na ZILE zitokanazo na mfuko wa jichangie, TFF inatoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania kuchangia mfuko huu ili utumike kunusuru mpira wetu. Fedha zitakazokusanywa matumizi yake yatasimamiwa na kanuni za uendeshwaji wa mfuko huu.
Hitimisho:
Kila mwanafamilia wa TFF anawajibika kuheshimu na kufuata maelekezo ya Kanuni za mashindano ya ligi kuu kama zilivyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF. Hivyo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na fedha za milangoni na za wadhamini kama ulivyoainishwa kwenye kanuni hizi uko pale pale. Ninaiagiza Bodi ya ligi kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya utendaji ya TFF mara moja. Mwenye malalamiko kuhusu kanuni hizi ayalete kwenye vyombo husika vya TFF kwa kufuata Katiba, kanuni na taratibu za Shirikisho.Sote tunajenga nyumba moja hakuna haja ya kugombea fito.
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Dar es salaam
02/October/2014