Bunge la Katiba Lapitisha Katiba Inayopendekeza, Pinda Ataka Ianze 2015

Bunge Maalum la Katiba

Bunge Maalum la Katiba


HATIMAYE Bunge Maalumu la Katiba limehitimisha kazi yake leo Mjini Dodoma na kutolewa kwa matokeo ya upigaji kura kwa wajumbe kuipitisha Katiba inayopendekezwa. Akisoma taarifa ya matokeo ya kura Bungeni leo, Naibu Katibu wa Bunge la Katiba, Dk. Thomas Kashililah alisema idadi kubwa ya wabunge wamepiga kura za ndiyo kupitisha Sura na Ibara zilizopigiwa kura na wabunge hao.

Alisema kura theluthi mbili za wajumbe wa Tanzania Bara na wale wa Tanzania Visiwani zimepatikana hivyo kwa mujibu wa katiba inayopendekezwa imepita kwa kura za kutosha na iliyobaki sasa ni Katiba hiyo kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya hatua nyingine za kupigiwa kura.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta akisoma taarifa rasmi kwa wabunge ya Bunge hilo kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa kura za kutosha, aliwapongeza wabunge kwa ushirikiano na uzalendo waliouonesha hadi kumalizika kwa bunge hilo likiwa na mafanikio ya kutoka na Katiba inayopendekezwa.

Sitta alisema kwa mujibu wa utaratibu tayari Sekretarieti ya Bunge hilo maalum imeandaa utaratibu wa kufanya makabidhiano ya Katiba hiyo kwa marais wote wawili. Sitta alisema Oktoba 10, 2014 Bunge hilo litamkabidhi Rais Jakaya Kikwete Katiba hiyo inayopendekezwa katika hafla itakayofanyika Mjini Dodoma. Alisema wabunge wa Bunge Maalum wote walioshiriki kukamilisha kazi hiyo watapewa vyeti maalum vya heshima kutambua mchango wao katika kazi hiyo.

Akizungumza kabla ya kufungwa kwa Shughuli za Bunge hilo Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda alishauri zoezi la upigaji kura kwa wananchi kupitisha Katiba hiyo inayopendekezwa lifanyike haraka ili kama inawezekana Rais wa Tanzania ajaye aanze kazi kwa kutumia katiba mpya. Aidha Pinda alisema kukaa kimya kwa sasa kunaweza kusababisha watu wasio na mapenzi mema kuchochea vurugu na hatimaye kukwamisha mambo yenye nia njema.

Waziri Mkuu huyo ambaye alionekana kusisitiza amani na utulivu nchini alishauri kama ikiwezekana tutakapokuwa tukipiga kura ya Uchaguzi Mkuu wa Taifa ujao (2015) yafanyike mambo yote kwa wakati mmoja yaani kupiga kura ya Uchaguzi wa viongozi na papo hapo uchaguzi wa kuikubali ama kuikataa Katiba hiyo iliyopendekezwa. “…Mi nashauri kama itawezekana tutakapokuwa tukipiga uchaguzi mwakani tufanye mambo yote kwa wakati mmoja…mtu anachagua kiongozi na anapiga kura ya Katiba..,” alisema Pinda.

Haya hivyo aliwaomba Wanawake kuhakikisha wanahamasishana na kushawishiana ili kuipitisha katiba hiyo kwani idadi kubwa ya wapiga kura ni wakinamama na kama wakiamua jambo linaweza kufanikiwa. Alisema Katiba iliyopitishwa na Bunge hilo ni nzuri na endapo itapita inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa Watanzania na nchi kwa ujumla. Pinda aliwashukuru wabunge wa Bunge hilo kwa kuonesha uzalendo na kupuuza maneno yote ya chokochoko yaliyokuwa yanatolewa na baadhi ya watu kufifisha morali ya wajumbe kufanya kazi hiyo.

Kupitishwa kwa Katiba hiyo inayopendekezwa kunaruhusu utaratibu mwingine kuanza kufanyika ambapo Rais Kupitia mamlaka husika atatangaza utaratibu kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwawezesha Watanzania kupiga kura ama kuikubali Katiba hiyo au kuipinga kabla ya kuingia kwenye mchakato wa matumizi.