Barabara ya Mwenge-Tegeta Yagharimu Bilioni 77.85

 Sehemu ya barabara  ya Mwenge-Tegeta yenye urefu wa Km 12.9, ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Tanzania wa kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam. Picha na Ikulu.

 Sehemu ya barabara  ya Mwenge-Tegeta yenye urefu wa Km 12.9, ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Tanzania wa kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam. Picha na Ikulu.

BARABARA ya Mwenge-Tegeta ya jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilomita 12.9 imegharimu kiasi cha Sh. bilioni 77.85, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la JICA.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Oktoba Mosi, 2014, alipokuwa akizindua rasmi Barabara hiyo iliyojengwa kisasa ambayo ni sehemu ya Barabara ya New Bagamoyo Road. Serikali ya Tanzania imechangia asilimia 7.64 katika gharama za ujenzi wa Barabara hiyo.

Rais Kikwete amefanya uzinduzi huo katika eneo la Makutano ya Kambi ya Jeshi ya Lugalo na Barabara ya Kawe katika sherehe iliyoshuhudiwa na mamia ya wananchi. Alikuwa ni Rais Kikwete ambaye aliweke jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara hiyo Aprili 4, mwaka 2011.

Barabara hiyo ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa Barabara itokayo Makutano ya Barabara ya Kawawa, Kinondoni hadi Tegeta. Ujenzi wa awamu ya pili wa kilomita 4.3 kati ya Mwenge na Makutano ya Barabara ya Kawawa, unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya mipango yote ya ujenzi huo kukamilika.

Barabara hiyo ya Mwenge-Tegeta inalenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo la kaskazini mwa Dar Es Salaam na pia ni sehemu ya bararaba kuu inayounganisha Jiji la Dar Es Salaam na Mkoa wa Pwani, kupitia Wilaya ya Bagamoyo, na kuunganisha mikoa hiyo na mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo ya uzinduzi wa Barabara hiyo iliyojengwa na Kampuni ya Konoike kutoka pia Japan, Balozi wa Japan katika Tanzania, Mheshimiwa Masaki Okada amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulichelewa kukamilika mwaka jana, kama ilivyopangwa, kwa sababu ya wajenzi kukabiliwa na matatizo ya mafuriko makubwa yaliyotokea mwaka 2011.

Mbali na kutaja misaada mingi katika sekta ya miundombinu na hasa barabara ambayo imefadhiliwa na Japan katika miaka mingi iliyopita, Mheshimiwa Okada amesema kuwa Japan sasa iko tayari kuanza ujenzi wa Barabara ya Gerezani-Bendera Tatu, Dar Es Salaam, utakaogharimu Sh. bilioni 18.5, msaada kutoka Japan.

Aidha, Balozi huyo amewaomba radhi Watanzania kutokana na ucheleweshaji wa kuanza kwa ujenzi wa barabara ya juu kwa juu –flyover- katika eneo la TAZARA, Dar Es Salaam, ambao utagharimu Sh. bilioni 53 ambazo zinatolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la JICA.

Amesema kuwa ujenzi huo umechelewa kwa sababu makandarasi wa Kijapan ambao walitakiwa kujenga flyover hiyo wanakabiliwa na kazi nyingi huko nyumbani za kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na kimbunga cha Great East Japan Earthquake and Tsunami, kilichotokea Machi 2011 na kusababisha uharibifu mkubwa mno. Aidha, amesema kuwa wajenzi hao pia wanalazimika kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miundombinu ya kuiwezesha Japan kuandaa Michezo ya Olimpiki ambayo imepangwa kufanyika nchini humo mwaka 2020.