JK Ataja Hatua Saba Zinazofanywa Kupunguza Msongamano Dar

Foleni ya magari jijini Dar es Salaam.

Foleni ya magari jijini Dar es Salaam.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametaja hatua saba ambazo Serikali yake imeanza kuzichukua ili kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa msongamano wa magari ni ishara ya ubora wa maisha ya wananchi na ustawi wa Watanzania kwa sababu miaka 20 ama hata 10 iliyopita, Jiji la Dar Es Salaam halikuwa na msongamano. “Sasa kila mtu ana gari, naambiwa nyumba nyingine zina magari matatu – la baba, la mama na la watoto.”

Hata hivyo, Rais Kikwete ameonya kuwa, kama ilivyo katika miji yote mikubwa duniani, ni jambo lisilowezekana kumaliza tatizo la msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar Es Sslaam (Central Business District), hasa kwa kutilia maanani kuwa hakuna shaka kuwa watu wataendelea kununua magari na huwezi kuvunja nyumba zote katikati ya Jiji ili kupanua barabara.

Rais Kikwete ambaye alikuwa anazungumza leo, Jumatano, Oktoba Mosi, 2014, wakati akizindua rasmi Barabara kisasa ya Mwenge -Tegeta kwenye Barabara ya New Bagamoyo Road, amezitaja hatua hizo za kukabiliana na msongamano wa magari katika Mji wa Dar Es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya Mabasi Yaendayo Kasi (DART), ambao awamu yake ya kwanza inakaribia kukamilika pamoja na uanzishwaji wa huduma za kisasa za usafiri wa treni katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.

“DART inalenga kuwashawishi wananchi kupunguza matumizi ya magari binafsi na kutumia zaidi usafiri wa umma. Na hili litawezekana ikiwa mabasi yenyewe yatakuwa mazuri na huduma ikawa bora,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Usafiri wa treni ambao nausema mimi ni usafiri wa treni za kisasa zenye mabehewa ya kubeba abiria mijini siyo ule wa sasa ambako mabehewa ya kwenda Kigoma na Mwanza ndiyo yanatumika kubeba abiria kati ya Dar Es Salaam na Tabata.”
Hatua ya tatu ambayo Rais Kikwete ameitaja ni kujengwa kwa barabara za juu kwa juu (flyovers) katika maeneo ya TAZARA na Ubungo, yenye msongamano wa watu wengi, na ujenzi wa barabara 12 za kuzunguka Jiji (Ring Roads) na nyingine za kuunganisha maeneo ya jiji hilo kama vile upanuzi wa Barabara ya Uhuru kuwa njia mbili kila upande badala ya njia moja ya sasa.

Aidha, Rais Kikwete amezitaja hatua nyingine kuwa ni ujenzi wa Daraja jipya la Salender ambalo litapitia baharini, usafiri wa kivuko kipya kutoka Bagamoyo hadi Dar Es Salaam na ujenzi wa miji midogo ya kisasa inayojitegemea katika maeneo ya Kigamboni, Mabwepande na Luguruni. Rais Kikwete amesema kuwa baadhi ya hatua hizo zinazochukuliwa ama zinalengwa kuchukuliwa na Serikali zimekuwa zinakabiliwa na siasa nyingi za kupinga miradi hiyo kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa nchini ambao amewaita “watu wenye upeo mfupi”.

“Kiongozi anayehubiri upinzani wa maendeleo kwa sababu za siasa ni kiongozi mbovu. Huyu ni mtu mwenye uongozi mbovu, na ana upeo mfupi, usiiona mbali, kwa sababu kiongozi mzuri hawezi kuhubiri siasa za kupinga maendeleo ya wananchi wake.”