Wabunge Waanza Kuipigia Kura Katiba Inayopendekezwa

Bunge Maalum la Katiba

Bunge Maalum la Katiba

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WABUNGE wa Bunge Maalum la Katiba wameanza kupiga kura kuipigia kura Rasimu ya Katiba inayopendekezwa baada ya kuwasilishwa kwao na Kamati ya Uandishi ya Wajumbe hao. Zoezi la kupiga kura hizo limeanza rasmi majira ya saa tisa za jioni ambapo mbunge mmoja baada ya mwingine wamekuwa wakiitwa kwa majina na mbunge huyo kupiga kura yake kwa njia anayoitaka yeye ama kwa wazi au kwa siri.

Wabunge wamekuwa wakiitwa kwa majina na kupiga kura zao kwa wale waliopo bungeni muda huu mara baada ya zoezi hilo kuanza huku bunge likiongozwa na Mwenyekiti wake Samuel Sitta, ambaye ameongoza bunge hilo jioni hii.

Hata hivyo kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa wabunge waliopo nje ya Bunge hilo pia watapiga kura zao kwa njia ya mawasiliano mengine chini ya usimamizi na muongozo wa Sekretarieti ya bunge la Katiba. Kwa mabadiliko hayo hata wabunge waliopo nje ya nchi watapata nafasi ya kupiga kura zao.

Jumla ya Sura 10 za Katiba hiyo inayopendekezwa na Ibara 157 ndizo zilikuwa zinapigiwa kura na wabunge wa bunge la Katiba, huku kila mmoja akipewa uhuru ama kupiga kura ya wazi au ya siri.

Pamoja na hayo idadi kubwa ya wabunge waliopiga kura za hadi muda huu ambapo zoezi la upigaji kura linaendelea wamepiga kura za wazi huku wengi wakionekana kubali kupitishwa kwa katiba hiyo inayopendekezwa yaani kura ya “Ndiyo”. Hata hivyo wapo waliokuwa wakipiga kura kwa siri pia. Kwa habari zaidi juu ya zoezi hili ni hapo baadaye kidogo hapa hapa www.thehabari.com.