Tanzania Ipo Tayari Kiushirikiano na UN Kutekeleza MDGs

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wajumbe katika Mkutano Mkuu wa 69 wa UN uliofanyika jijini New York.

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wajumbe katika Mkutano Mkuu wa 69 wa UN uliofanyika jijini New York.


TANZANIA iko tayari kushirikiana na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa (UN) kufikia makubaliano ya Malengo ya Maendeleo mapya baada ya Malengo ya Milenia (MDGs) ya sasa kufikia mwisho wake ifikapo mwaka 2015. Rais Kikwete amesema hayo wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jana tarehe 25 Septemba, 2014 jijini New York, Marekani.
Agenda ya kikao cha Baraza Kuu la UN mwaka huu ni “Delivering on and Implementing a Transformative Post 2015 Development Agenda” ambapo amesema anatarajia majadiliano yatatoa nafasi kwa nchi kupanga mipango ya baadae kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Tutumie muda huu kuendeleza mafanikio na mafunzo kutoka nchi mbalimbali na pia tujifunze kutokana na changamoto za kushindwa kufikia malengo ya Milenia, na kuzitumia kama viashiria vya ajenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015”. Rais amesisitiza.
Rais ameiasa dunia kuwa wakati huu ambapo inajadili ajenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015, isisahau malengo ya milenia ambayo hayajakamilika na kuyaweka vizuri katika ajenda mpya ya baada ya malengo ya sasa kufikia tamati mwaka ujao.
Pamoja na kwamba dunia inazungumzia ajenda mpya ya baada ya mwaka ujayo amezitaka nchi kuhakikisha na kuongeza kasi ya utekelezaji katika kipindi cha siku 461 zilizobakia kufikia mwisho. Pamoja na umuhimu wa MDGs Rais Kikwete amezungumzia suala la Tabia Nchi na kuzitaka nchi zote duniani kukusanya nguvu katika suala hili ili kuiokoa dunia kutokana na majanga ya Tabia Nchi.
Masuala mengine ni kuhusu Mageuzi katika UN, ambapo Rais Kikwete amesema kusuasua kwa mazungumzo ya kuleta Mageuzi kunakatisha tamaa na kuomba yafufuliwe. Masuala mengine ni kuhusu hali ya usalama duniani ambapo ugaidi umechukua mkondo wa kutishia amani duniani na kuzitaka nchi zote kupambana na ugaidi.
Masuala mengine ni pamoja na suala la muda mrefu la uhasama baina ya Israeli na Palestina ambalo limedumu kwa muda mrefu hivyo kuutaka Umoja wa Mataifa kulitafutia suluhu ya kudumu.
Suala lingine ni la Sahara Magharibi ambalo pia limedumu kwa muda mrefu bila ufumbuzi, suala la vikwazo kwa nchi ya Cuba ambavyo navyo vimekuwepo kwa muda mrefu sana, hivyo kuutaka Umoja wa Mataifa kutafuta utatuzi wa kudumu.
Rais Kikwete pia amezungumzia ugonjwa wa Ebola ambao tayari umeua watu wapatao 2,400 na bado haujadhibitiwa. Rais amesema ugonjwa wa Ebola ni tishio kwa nchi zilizoathirika, jirani na dunia kwa ujumla.
“Juhudi za pamoja zinahitajika kwani ndiyo njia sahihi, naamini kuna teknolojia na rasilimali za utaalamu na fedha ambavyo kwa pamoja,tunaweza kushinda tishio la ugonjwa huu” amesema.
Rais amezitaka juhudi zaidi zifanyike katika kuudhibiti, kwa kuwa ugonjwa huu ni hatari na unaweza kuwa janga la dunia.