MUUGUZI Jackson Namunya Tali (41) nchini Kenya amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumtoa mgonjwa mimba iliyosababisha kifo baada ya kuvuja damu nyingi mfululizo.
Hukumu hiyo kali kutolewa nchini kenya kwa makosa kama hayo imetolewa na Jaji Nicholas Ombija wa Mjini Nairobi, Muuguzi Tali kupatikana na kosa la kusababisha kifo cha msichana, Christine Atieno katika Kituo cha Afya anachosimamia. Nchini Kenya kitendo cha kutoa mimba ni kinyume cha sheria ingawa baadhi ya matabibu hufanya shughuli hizo kwa kutokana na wahusika kutoa pesa nyingi katika huduma hiyo.
Kulingana na taarifa ya mashahidi, Msichana Atieno alitunga mimba bila kutarajia mwezi Julai, 2009 na kuamua kutafuta msaada kwa Tali katika kituo chake cha afya kilichopo eneo la Gachie, viungani jijini Nairobi ambapo alitaka kuitoa mimba hiyo.
Mashahidi walieleza kwamba licha ya jaribio la kuitoa mimba hiyo kufanyika haikutoka na badala yake mtoto aliyekua tumboni kufa, hali iliyosababisha marehemu kuvuja damu nyingi. Mshtakiwa alipogundua hali hiyo mbaya kwa mteja wake alianza kumpa madawa ya kutuliza maumivu, kisha akampeleka katika Hospitali ndogo ya Kaunti ya Kiambu.
Wahudumu wa afya katika hospitali ya Kiambu walishauri mgonjwa huyo kupelekwa katika hospitali nyingine kwa matibabu maaluum ambapo angepokea matibabu ya dharura kwani hali yake ilikua mbaya. Hata hivyo msichana huyo, ambaye wakati huo wote alikuwa akivuja damu akiwa ndani ya gari la mshtakiwa alifariki dunia na muuguzi aliyemhudumiwa kulaumiwa kwa kifo hicho na kushtakiwa.
Nchini Kenya kutoa mimba haikubaliwi isipokuwa madaktari watathibitisha kwamba maisha ya mama yako hatarini. Mjadala ya kuhalalisha utoaji mimba umevuta hisia kali nchini Kenya kati ya wanaounga wakisema itasaidia afya ya uzazi huku wapinzani wakisema ni mauaji ya kiumbe asiye na hatia.
-BBC