MABADILIKO ya Tabia Nchi duniani yanahatarisha Uhai na Maendeleo ya Binadamu, ikiwemo kurudisha nyuma au kufuta kabisa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii yaliyokwishapatikana. Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo 23 Septemba, 2014, jijini New York, Marekani wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo amewakilisha msimamo wa bara zima la Afrika kuhusu suala zima la Tabia Nchi.
Rais Kikwete ametahadharisha kuwa kama hali iliyopo sasa hivi haitashughulikiwa, madhara yake yatakuwa makubwa hivyo dunia inapaswa kuchukua hatua za kukabiliana na Tabia Nchi. Rais Kikwete anasema, Afrika inaamini kuwa hali hii inaweza kubadilishwa kwa sababu wazalishaji wakubwa wa hewa ya ukaa ni nchi zilizoendelea ambazo zina teknolijia, ujuzi wa kiufundi, na uwezo wa kifedha kuchukua hatua zinazostahili.
“Sote tunajua kuwa hiki ndicho kimetamkwa na Mkataba wa Kyoto na itifaki zake na tunachosisitiza hapa ni kuwa, makubaliano haya yaheshimiwe na kutekelezwa” Amesema.
Pamoja na mambo mengine, Mkataba wa Kyoto umezitaka nchi ambazo zinazalisha kwa wingi hewa ya ukaa, kuchukua majukumu zaidi ya kupambana na athari za Tabia Nchi. Katika utaratibu huo, nchi za Afrika zinachangia kiasi kidogo sana cha hewa ya ukaa na uchafuzi wa Mazingira kwa ujumla.
Mkutano huo kuhusu Tabia Nchi umeongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Ban Ki Moon. Mapema akihutubia Baraza la UN Rais Baraka Obama wa Marekani amesema kuwa tishio la Tabia Nchi ni la dunia nzima na kuelezea kuwa madhara ya Tabia Nchi yanaongezeka haraka kuliko hata hatua zake za kukabiliana nayo na hivyo dunia inatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuahidi kuwa Marekani itazisaidia nchi zinazoendelea kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Viongozi wakuu duniani wamekwisha wasili jijini New York Marekani ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litaanza kusikiliza hotuba na misimamo ya nchi wanachama kuanzia leo tarehe 24 – 27 Septemba, 2014 na mijadala inatarajiwa kuanzia tarehe 29 Septemba.
Masuala makubwa yatakayojadiliwa katika kikao cha Baraza Kuu la UN mwaka huu ni pamoja na kuzungumzia changamoto mbalimbali duniani zikiwemo za umaskini, njaa, usalama na mabadiliko ya Tabia Nchi. Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia Baraza hilo tarehe 25 Septemba,2014 kati ya Saa 11 hadi Saa 1 na nusu usiku, (Tanzania iko mbele kwa masaa 7). Hotuba hiyo inaweza kuonekana moja kwa moja kupitia UN webcast.