JWTZ Jeshi Bora Lenye Weledi na Ujuzi Afrika

Baadhi ya vifaa vya kisasa na vikosi vya JWTZ.

Baadhi ya vifaa vya kisasa na vikosi vya JWTZ.

Baadhi ya vifaa vya kisasa vya JWTZ katika maonesho.

Baadhi ya vifaa vya kisasa vya JWTZ katika maonesho.

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), ambalo mwezi huu limetimiza umri wa miaka 50 tokea kuanzishwa kwake Septemba Mosi, mwaka 1964, ni miongoni mwa majeshi bora na yenye weledi, uzoefu na ujuzi mkubwa wa mapambano katika Bara la Afrika na nje ya Bara hilo.
Kwa hakika, Kikosi cha Majeshi Maalum (Special Forces) cha TPDF kinacholinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kimeelezwa kuwa miongoni mwa vikosi bora 30 vya majeshi maalum duniani kwa mafunzo, uwezo na weledi.
TPDF lilihitimisha sherehe za miaka 50 ya uhai wake kwa Onyesho la Medali la Operesheni Maliza Matata lililofanyika kwenye eneo la mafunzo la Jeshi hilo la Langururusu, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha, ambako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mgeni rasmi.
Matukio yaliyopelekea kuzaliwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania yalianza Januari 20, mwaka 1964, wakati jeshi la wakati huo la Tanganyika Rifles lililokuwa limeachwa na Wakoloni wa Kiingereza lilipofanya uasi dhidi ya Serikali ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika madai yao, askari hao wa Tanganyika Rifles walitaka kuongezwa mishahara, kuboreshwa kwa mazingira yao ya kazi, kupandishwa vyeo na kuondolewa kwa maofisa wa Kizungu, ambao wakati huo ndio walikuwa viongozi wa jeshi hilo.
Januari 25, mwaka huo huo wa 1964, Mwalimu Nyerere alitangaza kuvunjwa kwa jeshi hilo la Tanganyika Rifles na akafanya uamuzi wa kuundwa kwa Jeshi jipya la kuchukua nafasi ya Tanganyika Rifles.
Jeshi hilo la Kikoloni lilipewa jina la Tanganyika Rifles kufuatia uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961. Kabla ya hapo, Jeshi la Tanganyika liliitwa King African Rifles, jina lililoashiria utiifu kwa Mfalme wa Uingereza na lililoanza kutumika tokea mwaka 1918 wakati Waingereza walipoanza kuitawala Tanganyika kufuatia Vita Kuu ya Pili la Dunia.

Mkuu wa JWTZ, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ), Generali Devis Mwamunyange (kushoto) akivishwa moja ya nishani na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Mkuu wa JWTZ, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ), Generali Devis Mwamunyange (kushoto) akivishwa moja ya nishani na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Kwa hakika, historia ya majeshi katika Tanzania inaonyesha kuwa jeshi la kwanza la Kikoloni kuanzishwa nchini lilianzishwa na Wakoloni wa Kijerumani mwaka 1891 na liliitwa Germany East African Army wakati huo Wajerumani wakitawala nchi za Tanganyika, Burundi na Rwanda kama nchi moja iliyoitwa Detsche East Africa.
Kufuatia uamuzi wake wa kuvunja Tanganyika Rifles, Mwalimu Nyerere aliwachukua vijana 1,000 wanachama wa vijana wa chama cha TANU wa TANU Youth League kuandaliwa na kupewa mafunzo ya kijeshi na Septemba Mosi, mwaka huo huo wa 1964, vijana hao waliunda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Katika kuunda TPDF, Rais Nyerere alilipa Jeshi hili jipya shabaha namalengo ya msingi manane ambayo yameongoza shughuli za Jeshi hilo katika miaka 50 iliyopita – yaani tokea 1964 hadi 2014.
Tokea kuanzishwa kwake hadi sasa, Jeshi ya Wananchi halijawahi kuacha misingi, shabaha na malengo hayo. Limebakia kuwa Jeshi la Ulinzi wa nchi na siyo uvamizi, limebakia kuwa Jeshi linalotokana na Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya Wananchi wa Tanzania na pia limebakia kuwa Jeshi la kulinda amani duniani na kushiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi.
Shabaha na malengo ya msingi ambayo Rais Nyerere alilipa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni kama ifuatavyo:
• Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
• Kulinda Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
• Kufanya mafunzo na mazoezi ili kujiweka tayari kivita wakati wote
• Kufundisha umma shughuli za ulinzi
• Kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa
• Kutoa huduma mbali mbali za kijamii
• Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na
• Kushiriki ulinzi wa amani na shughuli za ukombozi wa Afrika.
Katika miaka yote 50 ya uhai wake, siyo tu kwamba TPDF imetekelezwa ipasavyo malengo na shabaha zake za msingi kikwelikweli, lakini pia TPDF limebakia jeshi imara, lenye uzalendo, lenye utii na nidhamu ya hali ya juu.
Kama alivyosema Rais Kikwete wakati wa sherehe za miaka 50, “Hizi ni sifa ambazo mataifa mengi hususan katika Afrika zimeshindwa kufanikisha, Tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa amani, utulivu na usalama wa nchi yetu katika miaka yote 50 umechangiwa sana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.”
• Jeshi la TPDF limelinda ipasavyo mipaka ya Tanzania na uhuru wake kwa vitendo kwa kuyapiga na kuyambaratisha kabisa majeshi ya uvamizi ya Idd Amin wa Uganda katika vita ya 1978/79 ambalo kwa mara ya kwanza jeshi la nchi moja limelipiga kabisa jeshi la nchi nyingine na kulifuta kabisa. Shughuli hii iligharimu maisha ya wanajeshi wa Tanzania.

• TPDF limeshiriki kikamilifu kufanikisha harakati za ukombozi barani Afrika kwa kufundisha majeshi ya vyama vya ukombozi, kushiriki moja kwa moja kwenye vita vya ukombozi Kusini mwa Afrika na kuchangia kupatikana kwa uhuru wa Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini. Kama ilivyokuwa vita dhidi ya Amin, vita vya ukombozi pia viligharimu maisha ya baadhi ya askari wa TPDF.

• TPDF limeendelea kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani duniani na kupata mafanikio makubwa kwenye operesheni za kulinda amani katika Liberia, Darfur (Sudan), Lebanon, Ivory Coast, Visiwa vya Shelisheli, Visiwa vya Comoro na sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako majeshi hayo yamekiangamiza kabisa kikundi cha waasi wa M23.

Baadhi ya vikosi vya JWTZ katika shughuli anuai za taifa.

Baadhi ya vikosi vya JWTZ katika shughuli anuai za taifa.

• Majeshi ya TPDF yameshiriki kikamilifu kwa kushirikiana na mamlaka za kiraia katika uokoaji na maafa hususan majanga yakiwemo – ajali ya MV Bukoba, ajali ya meli Zanzibar, mafuriko ya Kilosa, Morogoro, ambako Jeshi lilitengeneza hata reli iliyokuwa imezolewa na mafuriko hayo.

Moja ya mzinga wa kisasa wa JWTZ.

Moja ya mzinga wa kisasa wa JWTZ.

• Jeshi la Ulinzi la Wananchi limeendelea kutoa huduma mbali mbali za kijamii katika sekta za elimu na afya. Watanzania wengi wamenufaika na shule na hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Jeshi katika maeneo mbali mbali nchini.

• Kupitia JKT na JKU, Jeshi la Wananchi limekuza na kuendeleza elimu ya kujitegemea kwa vijana wa Tanzania.

• Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetoa mafunzo ya kijeshi kwa umma wakati wote wa kuwepo kwake na hasa kuanzia miaka ya mwanzo ya 1970 wakati lilipoanzishwa Jeshi la Akiba la Mgambo. Kufuatia kuanzishwa kwa Jeshi hilo la akiba, TPDF sasa ina mshauri wa mgambo katika kila mkoa na kila wilaya ya Tanzania.
Kutokana na umuhimu wake wa kipekee katika ulinzi wa maslahi ya Tanzania na Watanzania, Serikali nayo imedhamiria kuendelea kuliimarisha Jeshi kwa kuwekeza fedha na raslimali nyingine ili kuliweka katika utayari wa kivita kwa ununuzi wa vitendea kazi zikiwemo silaha za kisasa, usafiri na kuboresha maslahi na huduma bora kwa wanajeshi.
Serikali inaendelea kutambua wajibu wake wa kuwekeza katika ujenzi wa Jeshi bora wakati wa amani, kama historia ilivyokumbuka wakati wa uvamizi wa Idd Amin.
Ukweli huo ulisisitizwa na Mwalimu Nyerere katika hotuba yake wakati wa Sherehe za Mashujaa Septemba Mosi, 1979, wakati alipowapokea wanajeshi la Tanzania waliokuwa wanarejea kutoka vitani Uganda. Alisema Mwalimu:
“Vita sasa vimekwisha. Lakini kusema hivyo si kusema kuwa twaweza kulegeza mikanda. Hatuna wazo lolote la kumvamia mtu yoyote. Lakini ni vyema kuwa tayari kwa lolote linaloweza kutokea. Hilo ni funzo moja kubwa tulilolipata kutokana na vita hii.”