Ilala Kudhibiti Uzito wa Magari, Kujenga kwa Zege Barabara…!

Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Bi. Tabu Shaibu akiwaeleza waandishi wa Habari (Hawapo pichani) waandishi wa Habari kuhusu Miradi iliyotekelezwa kwa ajili ya kupunguza msongamano katika halmashauri hiyo, wakati wa mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari, Frank Mvungi. HASSAN SILAYO - MAELEZO.

Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Bi. Tabu Shaibu akiwaeleza waandishi wa Habari (Hawapo pichani) waandishi wa Habari kuhusu Miradi iliyotekelezwa kwa ajili ya kupunguza msongamano katika halmashauri hiyo, wakati wa mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari, Frank Mvungi. HASSAN SILAYO – MAELEZO.

Na Mwandishi Wetu, Dar

HALMASHAURI ya Ilala imepanga kuunda kitengo kitakachodhibiti uzito wa magari kwa kuweka mizani zinazohamishika katika maingilio yote ya barabara kuu za kuingia ndani ya halmashauri hiyo kudhibiti magari yanayozidisha uzito na huharibu barabara.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Uhusiano wa halmashauri hiyo, Tabu Shaibu na kuongeza kuwa kitengo hicho maalumu kitafanya kazi kwa masaa 24 ili kuzilinda barabara zake na wale wote wanaokiuka utaratibu na kuzindisha uzito kwenye barabara hizo.

“…Mikakati ya halmashauri ni kuunda kitengo kitakachodhibiti uzito wa magari kwa kuweka mizani zinazohamishika katika maingilio yote ya barabara kuu za kuingia katikati ya Halmashauri kwa masaa 24,” alisema Ofisa Uhusiano huyo.

Alisema halmashauri hiyo pia imedhamiria kujenga barabara ya zege eneo la Hydari Plaza ambalo limekuwa likiharibika kila mara kutokana na chemchem za maji ambazo zimekuwa zikiiharibu barabara hiyo kila mara.

“… Halmashauri inaendelea na maandalizi ya kuweka zege badala ya lami ili eneo hilo liweze kupitika kwa urahisi. Kazi hii itafanyika mapema katika mwaka huu wa fedha yaani 2014/2015. Hii ni kutokana kwamba halmashauri imekuwa ikiziba viraka vya lami bila mafaikio,” alisema Shaibu.

Aidha alifafanua kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia Idara ya Ujenzi inahudumia barabara zenye urefu wa kilomita 536.9 ambazo kati ya hizo kilomita 144.2 ni za lami, kilomita 64.7 ni za Changarawe na kilomita 328 ni za udongo.

Aliitaja miradi iliyokamilika hadi sasa ni ujenzi wa Barabara ya Mazengo hadi Kibasila kwa kiwango cha Lami Km.1.2, Ujenzi wa Barabara ya Lindi kwa kiwango cha Lami Km. 0.7, Ujenzi wa barabara ya Vingunguti Baracuda- urefu wa 1.3 km ambao unaendelea kwa sasa huku ikiwa tayari mita 880 ziko hatua kuanza kuweka lami nyepesi na lami ngumu.

“ Halmashauri imeweza kutekeleza kazi za uchongaji wa barabara za udongo na changarawe kwa kutumia greda lake moja. Barabara zilizochongwa ni za maeneo ya kata za Ukonga, Pugu, Majohe, Kivule, Msongola, Chanika, Kitunda, Kinyerezi, Tabata, Kimanga, Gongolamboto, Kipawa, Kiwalani, Vingunguti, Upanga Mashariki, upanga Magharibi, Gerezani Ilala, Jangwani, Mchikichini na Buguruni.”

“Barabara hizi zimekuwa zikiharibika wakati wa kipindi cha mvua zinapokuwa nyingi mathalani mvua zilizonyesha katika Mkoa wa Dares Salaam na kuleta maafa. Barabara nyingi ziliharibika kiasi cha kutopitika kabisa hali iliyoathiri huduma mbalimbali. Kwa kuliona hilo na kuhakikisha kuwa Barabara hizi zinapitika wakati wote Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imenunua Magreda mawili (2) kwa gharama ya Tshs 1.2 billioni. Pamoja na jitihada hizo yapo maeneo mawili ambayo kwa sasa ni kero,” alisema Ofisa Uhusiano huyo.