Mapya Yaibuka Ugonjwa wa Ebola

Mapya Yaibuka Ugonjwa wa Ebola
SIERRA Leone imesema kuwa imegundua visa vipya 130 vya maambukizi ya Ebola katika siku tatu ambapo Serikali iliweka amri ya kutotoka nje ikiwa ni hatua ya kupita mitaani kutoa elimu na kuwatambua wagonjwa majumbani.

Baada ya zoezi hilo jumla ya watu wengine 39 wametengwa huku wakifanyiwa uchunguzi kubaini ikiwa wameambukizwa ugonjwa huo. Mkuu wa kitengo cha dharura cha kukabiliana na ugonjwa huo, Stephen Gaojia, alisema kuwa amri ya kutotoka nje imefanikisha juhudi dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo.

Serikali ya nchi hiyo iliamrisha raia wake milioni sita kukaa majumbani kwa muda wa siku tatu katika juhudi za kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa Ebola. Ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu mbili na miasaba katika kanda ya Afrika Magharibi tangu mwezi Machi.
-BBC