WALIONUFAIKA NA MRADI WA WEZA, WAPATA MWAMKO WA KUDAI HAKI

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya

Na Mwandishi Wetu

JUMLA ya kesi 42 za ukatili dhidi ya wanawake vijijini huko Kusini Unguja na kaskazini Pemba zimefikishwa katika vyombo vya sheria.

Kesi hizo zinahusu wanaume waliooa na kuwatelekeza watoto na wake zao, mimba za utotoni, ubakaji na waume kupiga wake zao.

Taarifa hiyo imetolewa na Ofisa Mwezeshaji wa Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (WEZA) unaohusisha Shehia 60, Asha Abdi Makame ambaye alibainisha kuwa kesi 22 zimetokea Pemba na 20 kutoka Unguja.

Amesema makosa yanayoongoza ni yale kutelekezwa watoto na wanawake ambayo ni 36, yakifuatwa na makosa manne ya ubakaji na mawili ya kupigwa kwa wanawakeke ambayo yametokea Kusini Unguja katika shehia za Mtende na Kiboje Mkwajuni.

Mwezeshaji huyo wa WEZA amesema kesi 22 tayari zimeshatolewa maamuzi ya kisheria na zilizobaki ziko katika hatua tofauti kwenye vyombo vya sheria.

Mratibu wa shehia ya Nganani,Unguja mkoa wa kusini Bi Nyachum Mussa Haji ameiambia TAMWA kuwa hivi sasa wanawake wengi wamefahamu haki zao na hivyo kuchukua hatua haki zao zinapovunjwa.

“Tunashukuru kwamba hivi sasa tumekuwa na uelewa wa kuweza kuripoti vitendo vya udhalilishaji tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma” alisema Nyachum.

Hata hivyo wanawake hao walieleza kusikitishwa kwao kwa kuwepo kwa udhaifu wa sheria na tabia ya kuficha siri kuwa yanakosesha wanawake na wanaume wengi vijijini i haki zao za kisheria.

Shemsa Hassan kutoka shehia ya Kibuteni,Kusini Unguja aliyataja mapungufu hayo kuwa ni kutokuwepo kwa mashine ya kupimia vinasaba (DNA), kutokuwepo na sheria ya kubana wazazi kutokuozesha watoto wa kike hadi wanapomaliza elimu ya lazima, na kukosekana kwa sheria inayotoa ufafanuzi sahihi kuhusu mgawanyo wa mali za familia.

Alisema suala la mali ya familia linawaathiri sana wanawake ambapo huishia kunyan’ganywa kila kitu na waume zao mara baada ya ndoa kuvunjika.

“Sisi tuliwahi kupeleka kesi katika mashirika ya kutetea haki za wanawake na kuambiwa kabisa kuwa ni vigumu kwa wanawake kupata haki zao kutokana na kutokuwepo sheria mahususi na uhaba wa ushahidi kuwa mwanamke alishiriki katika ujenzi wa mali ya familia”, alisema.

Jumla ya wanavikundi 7,686 wanawake na wanaume wa mradi wa WEZA wamenufaika na mafunzo ya haki za binaadamu na sheria.

Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa mashirikiano kati ya Care Tanzania na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU)na Serikali ya Austria pamoja na Care Austria.