Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Ali Seif Idi ameshauri Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) uhakikishe kuwa shughuli zake zinaelezwa na kueleweka kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi visiwani humo ili kuufanya mpango huo ueleweka vyema.
Balozi Seif alitoa ushuri huo alipotembelea Banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Maonesho ya Wakulima, Nane Nane, yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni, Dodoma. Katika maonesho hayo, Wizara hiyo inaeleza shughuli zake sanjari na taasisi zake za APRM, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) na Chuo cha Diplomasia.
Awali akimweleza Makamu huyo juu ya utekelezaji wa shughuli za APRM hapa nchini, Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas alisema mpango huo ulikuwa ukafanye semina elimishi na ya uhakiki wa ripoti kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar lakini mchakato huo ukaahirishwa kwa kuwa ripoti inayoeleza Hali ya Utawala Bora nchini ililazimika kwanza kuhusishwa upya ili iwe na takwimu za karibuni.
“Ripoti ya awali iliyokamilika mwaka 2009 ilishindikana kukaguliwa na wataalamu toka nchi nyingine za Afrika kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kuzifanya baadhi ya takwimu zake zipitwe na wakati. Hivi sasa tunajiandaa kuizindua ripoti mpya iliyohuishwa katika semina kubwa itakayofanyika Agosti 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam,” alisema Bw. Abbas na kuongeza kuwa mara baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo semina hiyo na hata ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano zinaweza kufanyika.
Balozi Idi ambaye ndiye Kiongozi wa Shughuli za Serikali kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar alisema semina hiyo ni muhimu ili kuwapa fursa nyingine wajumbe wa Baraza hilo kufahamu mchakato huo. Alisema yeye binafsi pia angependa kuona jambo hilo linafanyika.
APRM ni mpango endelevu uliobuniwa na marais wa Afrika katika kikao chao cha mwaka 2002 ambapo walikubaliana kuweka utaratibu wa kila nchi kuanzisha taasisi hiyo na kisha kuipa jukumu la kufanyakazi ya kujitathmini mara kwa mara katika nyanja za utawala bora. Mkataba huo wa Afrika unaonesha kuwa nchi hutathminiwa kila baada ya miaka minne.
Taarifa zinaoneshan kuwa tayari nchi kadhaa za Afrika za Kenya, Rwanda na Ghana, zilikwishafanya hivyo na sasa zinarudia tena utafiti huo kwa mara ya pili ili kubaini changamoto mpya na kuzifanyikakazi. Tanzania sasa inakaribia kualika wakaguzi kutoka nje watakaokuja nchini Septemba mwaka huu na kisha Rais kuiwasilisha ripoti hiyo mbele ya wakuu wenzake wa Afrika na nchi kuanza kufanyiakazi changamoto zilizojitokeza.