Wabunge Wanawake Wasisitiza Usawa wa Kijinsia Katiba Mpya

wabunge wanawake

wabunge wanawake

Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.

KATIKA JUHUDI za kuleta usawa wa kijinsia na kuinua hadhi ya wanawake, Serikali imefanya jitihada kubwa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali katika jitihada hizo

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana wakati wa semina iliyohusu masuala ya kuwapa nyenzo ama uwezo wananawake waweze kushiriki vizuri katika maeneo mbalimbali yanayowakilisha wanawake huku wakiungwa mkono na wanaume.

Chana amesema kuwa baadhi ya watu nchini wamekuwa na dhana tofauti huku wakiona wakipotezewa muda pindi mambo yoyote yanayowahusu wanawake yanapozungumzwa wakisahau kuwa ili taifa liweze kufika mahali pazuri na kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania hakunabudi kulitazama kundi hilo la wanawake ambalo ni muhimu.

Ameeleza kuwa asilimia 51% ya Watanzania ni wanawake ambao wanachangia nguvu kazi kwa upande wa kilimo kwa asilimia 45 ya pato la Taifa, pia asilimia 25 wako katika ajira iliyo rasmi lakini wengi wako katika sekta isiyo rasmi.

“Asilimia 34% pia ya wanavyuo kutokana na takwimu inaonyesha kwamba ni wanawake, kwahiyo ajenda ya wanawake haikwepeki”, alisema Mhe. Chana.

Akizungumzia kuhusiana na masuala ya mchakato wa kusaka Katiba Mpya, Mhe. Chana amesema kuwa katika majadiliano yanayohusu Katiba, ajenda ya wanawake pia haikwepeki.

Aliongeza kuwa endapo wanawake nchini watawezeshwa basi taifa zima litakuwa limewezeshwa kwani watu wengi waliopata mafanikio ni kutokana na wanawake kutoa malezi bora katika kulea watoto pindi wanapozaliwa hadi kupata elimu.

Aidha, Chana amesisitiza juu ya wanawake kushirikishwa katika vyombo vya maamuzi ili kuongeza hali ya uchumi kwa wanawake, hali ya kijamii ya wanawake na ya kisiasa kwa wanawake hao.

“Lazima tuwepo kwenye vyombo vya maamuzi kwani ndiko tunapopata haki zetu kwani huko pia ndiko tunapoweka bajeti ya serikali kuu, bajeti ya serikali za mitaa, kwahiyo tunaanza na vyombo vya maamuzi”, alisisitiza Mhe. Chana.

Naye Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya Mhe. Usu Mallya amesema kuwa Tanzania ina wanawake wenye sifa, na uwezo na maarifa kwenye maeneo yote kuanzia, udaktari, uhasibu, Wahandisi yakiwemo na maeneo mengine.

Ameongeza kuwa, ajenda ya kufikia Hamsini kwa hamsini kwa wanawake haina mjadala, hivyo wanawake wana haki ya kuhusishwa katika masuala ya ungozi kama ilivyo kwa wanaume.

“Mwanamke kwenye uongozi ni lazima aweze kuliko mwanaume, anatakiwa ajiwekee mikakati yake mwenyewe ya kujihudumia (selfcare) ili kuwa na muda wetu wenyewe”, alisema Bi. Mallya.

Bi. Mallya aliongeza kuwa wanawake wanapaswa kutambua kuwa ajenda inayohusu mapambano ni ajenda ya muda mrefu ndani ya maeneo yao ya uongozi.

Bi Mally alisisitiza kuwa, wanawake wajitahid kuwa wanasiasa kwenye vyama vya siasa, wawe wabunge pia wawe viongozi kwenye taasisi na binafsi ili kufanikisha suala lao la hamsini kwa hamsini.