SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jumamosi ya Septemba 13 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi litaendesha mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki kwa wadau wa mpira wa miguu Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura amebainisha mafunzo hayo yatafanyika Uwanja wa Taifa, na kushirikisha wasimamizi wa mechi, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na makatibu na maofisa habari wa klabu za Azam na Yanga.
Alisema washiriki wengine wa mafunzo hayo ni Meneja wa Uwanja wa Taifa na msaidizi wake, wasimamizi wa milangoni (stewards), waandishi wa habari wa Dar es Salaam maofisa usalama wa TFF.
Mafunzo hayo yatahitimishwa Jumapili ya Septemba 14 mwaka huu kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Azam na Yanga kuanzia saa 10 kamili jioni. Tiketi zimeanza kuuzwa jana (Alhamisi) kupitia M-Pesa, CRDB Simbanking na maduka ya Fahari Huduma.