Mama Kikwete Ashauri Kinyesi cha Binadamu Kitumike…!

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa CARMATEC  Ndugu Elifariji Makongoro kuhusu ujenzi wa mtambo huo na unavyofanya kazi.  

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa CARMATEC  Ndugu Elifariji Makongoro kuhusu ujenzi wa mtambo huo na unavyofanya kazi.
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akikata utepe huku akishirikiana na viongozi mbalimbali ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa mtambo wa wa 10,000 wa Biogas hapa nchini. Mtambo huo unaomilikiwa na Ndugu Bakari Seif na Mkewe Mwanaidi Said (wa pili na wa tatu kutoka kushoto). Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Ndugu Eliakim Maswi, kulia kwa Mama Salma ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Ndugu Mwantumu Mahizana. Aliyesimama kushoto ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kondo Ndugu Ramadhan Seleman akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa CARMATEC Ndugu Elifariji Makomgoro.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitembelea maonesho ya biogas yaliyofanyika katika Kijiji cha Kondo tarehe 10.9.2014. Mkurugenzi Mkuu wa CARMATEC Ndugu Elifariji Makongoro (kulia) akimpatia maelezo mbalimbali ya kazi zinazofanywa na shirika hilo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Mwantumu Mahiza. PICHA ZOTE NA JOHN LUKUWI.

Na Anna Nkinda – Maelezo

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete ameutaka uongozi wa Tanzania Domestic Biogas Programme (CAMARTEC) kuangalia uwezekano wa kutumia kinyesi cha binadamu kuzalisha Biogesi katika maeneo yasiyo na mifugo ya kutosha kwa kuwa utekelezaji wa program hiyo unaangalia wingi wa mifugo hususani ng’ombe na upatikanaji wa maji.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliitoa rai hiyo jana wakati wa uzinduzi wa mtambo wa 10000 wa kuzalisha Biogesi uliojengwa katika kijiji cha Kondo wilayani Bagamoyo ulioenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Biogesi nchini.

Aliitaja mikoa ya Lindi, Mtwara, Katavi na Kigoma kutofikiwa na program hiyo kwa kuwa haina mifugo ya kutosha na kusema kuwa kinyesi cha binadamu ambacho nacho ni moja wapo ya Biogesi ambayo inazalishwa kila siku na huzalisha Biogesi kwa wingi ukilinganisha na vyanzo vingine.

Mama Kikwete alisema matumizi ya Biogesi yanamkomboa mwanamke kwa kumsaidia kupunguza muda mrefu wa kutafuta kuni kwani wanawake wengi kwenye kaya zenye Biogesi wameweza kuwa na muda wa kutosha wa kuhudumia familia na kufanya shughuli nyingine za uzalishaji zinazowaletea maendeleo.

“Biogesi humkomboa mwanamke kutokana na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo hutoa moshi na kusababisha madhara mengi kwa afya ya mama na mtoto. Teknolojia hii inaweza kupika kwa muda mfupi, kupunguza gharama za kununua nishati ya kuni na mafuta ya taa.”

Biogesi inatoa mwanga mzuri ambao huwawezesha watoto kujisomea usiku na familia kufanya shughuli zingine za maendeleo. Hii inaiwezesha familia kuachana na matumizi ya kurunzi, vibatari, kandili na aina nyingine zinazotumika kutoa mwanga hasa katika mazingira ya vijijini,” alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi alisema matumizi ya jumla ya nishati yanafikia takribani asilimia 90 yanatokana na kuni na mkaa. Utafiti uliofanywa unaonyesha kufikia mwaka 2030 mahitaji ya kuni na mkaa yatakuwa mara mbili zaidi ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo matumizi yalikuwa ni takribani tani milioni 2.3.

Mahitaji hayo yameongezeka kutokana na kukua kwa miji, ongezeko la bei ya mkaa na kuni au uhaba wa upatikanaji wa nishati mbadala kama vile mafuta ya taa, umeme, vitofali vya tungamotaka na Biogesi.

Maswi alisema, “Siku ya Biogesi kitaifa ni mojawapo ya mkakati wa wizara wa kuhakikisha kwamba teknolojia inakuwa na kuenea kwa watanzania wengi walioko vijijini haswa wafugaji wa ng’ombe. Hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira kwani mojawapo ya visababishi vikuu vya ukataji wa miti ni matumizi ya mkaa mijini na kuni kwa ajili ya kupikia vijijini.

Alisema mitambo 10000 imeweza kuzalisha nishati kiasi cha MWh 86406, imepunguza ukataji wa misitu kwa tani 6199 na kuzalisha mbolea tani 50717 na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa tani 5136 iwapo mitambo hii itatunzwa itazalisha kwa zaidi ya miaka 30.

Naye Ofisa Kilimo wa kijiji cha Kondo Amoni Mlungwana alisema wanakijiji hao baada ya kujifunza kuhusiana na manufaa ya matumizi ya Biogesi wamehamasika kwani ni mradi rafiki kwa mazingira na baada ya kukamilika unaokoa gharama kubwa ya maisha na kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini. Alizitaja changamoto inayowakabili ni kutokuwa na mifugo ya kutosha kutokana na hali duni ya kipato inayowapelekea wananchi kutonufaika na mradi huo.

Mlungwana alisema, “Tunaomba tuwezeshwe kupata ng’ombe na ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya Biogesi kwa wingi ili tuondokane na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa na kuimarisha kilimo kwa kutumia mbolea hai na kutoa ajira kwa vijana kupitia ujenzi wa mitambo hiyo.”

Mama Kikwete aliahidi kuwachangia wanawake wa wilaya hiyo kujenga mitambo 10 ya Biogesi ambayo itawasaidia kupata nishati kwa ajili ya kupikia, mwanga na kusaidia utunzaji wa mazingira. Technolojia ya Biogesi ambayo inazalishwa kutokana na vinyesi vya wanyama na masalia ya mimea iliingia nchini miaka ya 1970 kwa ufadhili wa mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wa maendeleo hadi sasa mitambo 10000 imeshajengwa nchini na kuwanufaisha watanzania zaidi ya 60000 kwa kupata nishati ya kupikia na mwanga.