Chadema wafanya uamuzi mgumu, watimua madiwani wake watano Arusha

Mwenyekiti wa CHEDEMA Taifa, Freeman Mbowe

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KIKAO cha Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana kwa dharura Jumamosi na Jumapili mjini Dodoma kimefanya uamuzi mgumu kwa kuamua kuwafukuza uanachama madiwani watano wa chama hicho mkoani Arusha ambao wamedaiwa kupinga amri ya kamati hiyo.

Madiwani waliotimuliwa uanachama hivyo kupoteza moja kwa moja nafasi zao za udiwani mkoani Arusha ni pamoja na Estomih Mallah, John Bayo, Charles Mpanda, Rehema Mohamed na Reuben Ngowi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe inasema tayari madiwani hao wamejulishwa uamuzi huo na kinachofuata ni kujuliswa rasmi kwa barua.

“….Hivyo basi, kwa kutumia mamlaka ya Kikatiba Kamati Kuu imewafukuza uanachama madiwani watano wafuatao kwa kosa la kukataa kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu: i) Ndugu Estomih Mallah, ii) Ndugu John Bayo, iii) Ndugu Charles Mpanda, iv) Ndugu Rehema Mohamed, v) Ndugu Reuben Ngowi,” alisema Mbowe katika taarifa yake.

Awali alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo iliyoyatoa katika Mkutano wake wa Julai 17, 2011 iliyowataka madiwani wa CHADEMA Arusha kujiuzulu nafasi walizozipata pamoja na kuomba radhi kwa makosa waliyoyafanya kutokana na mwafaka uliofikiwa baina yao na madiwani wenzao wa TLP na CCM kwa kuwa chama hakikuridhia wala kuutambua mwafaka huo.

Taarifa ilieleza kuwa kuwa, kati ya madiwani 10 waliopewa maelekezo na Kamati Kuu, madiwani watano ndiyo walitekeleza maelekezo kikamilifu huku madiwani wengine watano wakigoma kufuata maelekezo hayo.

Amesema baada ya Kikao cha Kamati Kuu kupokea taarifa ya utekelezaji na kutafakari kwa kina juu ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati Kuu, na kuwapa nafasi ya kujieleza madiwani waliogoma kutii maelekezo iliamua kuchukua uamuzi huo wa kuwatimua.

“Kamati Kuu imezingatia kuwa madiwani wamekataa kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu. Aidha, Kamati Kuu imezingatia kuwa kitendo cha madiwani kukataa kutekeleza maagizo halali ya Kamati Kuu ni utovu mkubwa wa nidhamu na ni kuvunja maadili na kanuni za chama, na kinaenda kinyume na msingi mama wa CHADEMA wa uwajibikaji.

Aidha, Kamati Kuu ilipokea taarifa ya mazungumzo baina ya Mbowe, na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, juu ya nia na azima ya kumaliza tatizo la mgogoro wa umeya Arusha.

Taarifa imesema kuwa tayari Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Waziri Mkuu wamekubaliana kuunda Kamati ya Kitaifa ya kushughulikia mgogoro wa umeya wa Arusha itakayojumuisha wajumbe kutoka sehemu mbili zinazohusika katika mgogoro huu ambazo ni CCM na CHADEMA.

Pia Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano itaundwa haraka iwezekanavyo, na kwa vyovyote mgogoro wa u-meya Manispa ya Arusha ulikubalika uishe ndani ya mwezi mmoja tangu tarehe ya mazungumzo ya Mwenyekiti wa Taifa na Waziri Mkuu.

Uenyekiti wa Kamati ya Kitaifa utakuwa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Ndugu John Tendwa, na kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa ataratibu uundwaji wa Kamati hiyo ya Kitaifa.

Pamoja na hatua njema kuelekea kumaliza mgogoro wa umeya Arusha, Kamati Kuu ya CHADEMA imesema itaendelea kutomtambua rasmi Meya wa Arusha hadi pale mazungumzo yaliyoanishwa yatakapokamilika na mwafaka bayana kupatikana.