KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Septemba 7 mwaka huu na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika. Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote. Mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.
Pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili.
Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri. Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Hata hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi. Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura. Kuhusu pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake. Vilevile Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa kulipa ada hizo.
Pia Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi, vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi watakapolipa. Mashauri mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya kamati. Kamati inasisitiza kwa wanachama wa TFF kuheshimu mikataba.