Rais Atoa Pole Vifo vya Watu 36 Ajalini Mara, 16 Wahamishiwa Bugando

Waziri wa  Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka (kushoto), akimjulia hali mmoja wa majeruhi wa ajali ya mabasi mawili yaliyogongana juzi katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara, waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa huo. Watu 36 walifariki dunia na wengine zaidi ya 79 kujeruhiwa.  Picha na Beldina Nyakeke.

Waziri wa  Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka (kushoto), akimjulia hali mmoja wa majeruhi wa ajali ya mabasi mawili yaliyogongana juzi katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara, waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa huo. Watu 36 walifariki dunia na wengine zaidi ya 79 kujeruhiwa.  Picha na Beldina Nyakeke.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia vifo vya watu 36 vilivyotokea katika ajali ya barabarani Wilayani Butiama, Mkoa wa Mara, ambako pia watu 79 wameumia, baadhi yao vibaya.

Mara baada ya kupata taarifa hiyo iliyotokea, Septemba 5, 2014, Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Arusha, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, akielezea huzuni na masikitiko yake.

“Nimehuzunishwa mno na kusikitishwa sana na taarifa hii ya kutisha ya vifo vya watu 36 ambavyo vimetokea leo wakati mabasi mawili yalipogongana ana kwa ana katika eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama, mkoani mwako. Nakutumia salamu zangu za rambirambi pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuomboleza vifo vya Watanzania wenzetu ambao wameaga dunia yetu ghafla katika ajali hii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Nakuomba uwafikishie wafiwa wote pole zangu nyingi sana, ukiwajulisha kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, napenda uwajulishe kuwa naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema roho za marehemu.”
“Aidha, naungana nanyi wana-Mara kuwapa mkono wa pole na kuwaombea wote walioumia katika ajali hiyo waweze kupona haraka ili wapate nafasi ya kuendelea na shughuli zao za maendeleo.”

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Philip Kalangi ameviambia vyombo vya habari mkoani hapo kuwa marehemu wa ajali hiyo wameshatambuliwa, huku majeruhi 19 ambao hali zao bado ni mbaya wamehamishiwa Hospitali ya Bugando Mwanza kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo alisema kuwa kwa sasa vifo vimeongezeka kutoka 36 hadi kufikia watu 37 baada ya majeruhi mmoja kufariki jana.