Waziri Membe ainadi wizara yake kwa wananchi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard K. Membe (Mb.) jana mjini hapa (6 Agosti, 2011), ametembelea Maonyesho ya Nanenane.

Waziri Membe katika ziara hiyo alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali ya baadhi ya wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na taasisi zake, kikiwemo Kituo cha kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Chuo cha Diplomasia Dar es salaam na Mchakato wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Katika maelezo yake, Waziri aliwaeleza wananchi umuhimu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa kushiriki katika maonyesho ya kilimo na kusema kwamba ushiriki wake unalenga katika kujifunza mahitaji halisi ya wananchi katika sekta ya kilimo.

Alisema Wizara kama kiungo cha wananchi na nchi za Nje lazima iwe na uelewa mpana wa mahitaji ya wananchi katika sekta ya Kilimo ili Wizara iweze kuyatangaza na kuzitafutia masoko bidhaa zao na wawekezaji nje ya nchi.

Kuhusu kujipanga kwa Wizara kusaidia sekta ya kilimo, Waziri alisema mkakati umekuwa wizara kutafuta wawekezaji wenye nia ya kuongeza tija katika usindikaji, uzalishaji na utunzaji wa bidhaa zilizosindikwa.

“Ni lazima watanzania waondokane na kasumba ya kuuza bidhaa kama pamba badale yake wauze nguo au badala ya kuuza korosho pekee, wauze korosho na mafuta yake,” alisema Waziri Membe.

Aidha alitoa mfano wa mazao mengi ambayo huzalishwa Tanzania ambayo baada ya muda mfupi kuweza kuharibiwa na wadudu waharibifu na hivyo kufanya wakulima kutofaidika na nguvu ya jasho lao. Hata hivyo alisema ili sekta ya kilimo iweze kukua lazima miundombinu ikiwemo ya barabara na umeme lazima iboreshwe akigusia tatizo la umeme kwamba linaathili uzalishaji katika viwanda na hivyo kufanya wakulima washindwe kuuza zaidi bidhaa zao viwandani na kushindwa kuzalisha kwa wingi.

Katika Banda hilo la Wizara ya Mambo ya Nje wananchi pia walipata maelezo kuhusu kazi za Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Chuo cha Diplomasia Dar es salaam na Mchakato wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).