Kamati Bunge Maalum la Katiba Zaendelea Kuwasilisha Taarifa

Kamati Bunge Maalum la Katiba Zaendelea Kuwasilisha Taarifa

Na Benedict Liwenga na Magreth Kinabo, Maelezo – Dodoma
 
KAMATI za Bunge Maalum la Katiba Septemba 4, 2014 zimeendelea kuwasilisha taarifa zao mbele ya Bunge hilo. Baadhi ya kamati zilizowasilisha taarifa zao katika Bunge hilo ni Kamati Namba Mbili, Kamati Namba Tisa, Kamati na Kumi, Kamati Namba Nne, Kamati Namba 12, ambazo ziliwasilisha asubuhi hadi mchana. Mambo makubwa yaliyozungumzwa katika Bunge hilo yanahusu mambo mbalimbali yakiwemo ya Uongozi wa Bunge, ambapo wengi wapendekeza wabunge wanaweza kuchaguliwa Spika au Naibu Spika na Mbunge kutowajibishwa na wananchi.
 
Pia kigezo cha kugombea nafasi ya ubunge kikiwa ni kujua kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Katika uwasilishaji huo, Kamati Namba Nne ya Bunge hilo, iliwasilisha taarifa yake, ambayo ilisomwa na Gosbert Blandes, taarifa, ambapo katika Ibara ya 132 inahusu Spika na Mamlaka ya Spika. Wajumbe wengi wanapendekeza ibara hiyo ifanyiwe marekebisho kwa kumwondoa mbunge kuwa miongoni mwa watu wasioruhusiwa kushika madaraka ya Spika.
 
Aidha siku za kuwasilisha tamko rasmi kuhusu mali zimeongezwa kutoka siku thelathini hadi tisini. Ibara hiyo ndogo ya (2) sasa itasomeka kama; (2) Waziri, Naibu Waziri, Mbunge au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote yatakayotajwa na sheria za nchi kwa madhumuni ya Ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Spika.
 
Sababu za mapendekezo ni kumwezesha Mbunge kugombea nafasi ya Spika na kuongeza siku za kuwasilisha tamko rasmi kuhusu mali ili kuondoa uwezekano wa Spika kushindwa kufanya hivyo kutokana na ufinyu wa muda. Ibara ya 133, ibara hii inahusu ukomo wa Spika. Baada ya mjadala Wajumbe walio wengi walipendekeza kufanya marekebisho kwa kufuta aya ya (a) linaloweka sharti la kukoma kwa nafasi yake kutokana na kuchaguliwa kuwa mbunge. Sababu za mapendekezo haya ni kutoa fursa kwa wabunge kushika madaraka ya Spika na kuendelea kushikilia nafasi zao za ubunge.
 
Ibara ya 134, ibara hii inahusu Naibu Spika. Kamati imejadili kwa kina ibara hii kasha wajumbe walio wengi walikuwa na mapendekezo kuwa ibara ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa neno Mbunge katika Ibara ndogo ya (2). Ibara hiyo sasa itasomeka kama ifuatavyo; 134 (2) Waziri, Naibu Waziri au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote yatakayotajwa na sheria za nchi kwa madhumuni ya Ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Sababu za mapendekezo haya ni kuwawezesha Wabunge kuwa na sifa ya kuchaguliwa kuwa Spika.
 
Ibara ya 135, Ibara hii inahusu sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika. Kamati imejadili kwa kina kuhusu sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika. Baada ya mjadala wajumbe walio wengi walipendekeza kuifanyia marekebisho ibara hii. Lengo la marekebisho haya ni kutoa wigo mpana kwa watu wenye sifa za kuchaguliwa kuwa wabunge kuwa na haki ya kuchaguliwa kuwa Spika na Naibu Spika ilimradi wana shahada ya Chuo kikuu inayotambulika. Ibara hii sasa itasomeka kama ifuatavyo;
 
135 (1) (1) Mtu atastahili kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika endapo mtu huyo ana elimu ya shahada ya chuo cha elimu ya juu kinachotambulika kwa mujibu wa sheria za nchi; (2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), mtu atastahili kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika ikiwa ana sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mbunge.
 
Kamati Namba Kumi ya Bunge Maalum  nayo iliwasilisha taarifa yake kuhusu sura ya Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa sura ya tisa na sura ya kumi, ambayo ilisomwa na Dk. Dalaly Kafumu. Dk. Kafumu alisema katika suala la Uchaguzi wa wabunge, Ibara ya 124(4) ya Rasimu ya Katiba inazungumzia uchaguzi wa mbunge endapo kiti cha ubunge kipo wazi.
 
“Kamati yangu inaona kuwa ibara hii inalenga kufuta uchaguzi mdogo kwa kuwa ibara hii inatoa mwanya wa mtu kuteuliwa na kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, kutoka kwenye orodha ya majina ya wagombea iliyowasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.
 
“Kamati yangu haikubaliani na utaratibu huo, hivyo inapendekeza kwa utaratibu unaotoa haki ya mtu kugombea na kuchaguliwa kama ilivyo katika ya sasa,” alisema.
 
Utaratibu wa kutayarisha orodha ya majina uliotajwa katika ibara ya 124 wa kumpata mbunge haujawekwa bayana kwa maana ya kuainisha mfumo wa uwiano wa kura na idadi ya wagombea kwani inatakiwa kuwa sawa na idadi ya viti bungeni. Aidha, mfumo unaopendekezwa utaleta dhana ya “Mbunge mtarajiwa” hali inayoweza kuathiri demokrasia na hata utendaji wa kazi wa mbunge anayekuwa madarakani. Kutokana na sababu hizo, Wajumbe wamependekeza ibara ndogo ya (4) ifanyiwe marekebisho na kusomeka; “(4) Endapo Mbunge anayetokana na chama cha siasa atapoteza sifa za kuwa Mbunge kwa sababu yoyote isiyokuwa ya Bunge kumaliza muda wake, Tume Huru ya Uchaguzi itatangaza uchaguzi wa Mbunge katika Jimbo hilo, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii”.
 
Alisema katika Ibara ya 125 (1) b kuhusu sifa za kuchaguliwa kuwa mbunge kuwa elimu isiyopungua kidato cha nne. Wajumbe walio wengi wamekubaliana kuwa ibara hiyo ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa kiwango cha elimu kwa kuwa suala la kugombea nafasi yoyote ni la kidemokrasia, haipaswi mtu kuzuiwa kugombea kwa kigezo cha elimu, kwani ni haki ya Katiba.
 
“Hali kadhalika, Katiba haitakiwi kuweka kigezo chochote kinachokiuka haki za msingi za kuchaguliwa na kuchagua. Pili haki ya kuamua kama mgombea anafaa au hafai ni ya wapiga kura,wasizuiwe kikatiba kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua mtu wanayemtaka. Pia utaratibu huuu haupo duniani kote hata kwa nchi zilizona demokrasia iliyokomaa,” alisema Blandes.
 
Aliongeza kuwa wajumbe walipendekeza Ibara hiyo ifanyiwe marekebisho kwa kuweka cha kujua kusoma na kuandika na si kiwango cha elimu kama sifa ya msingi. Hivyo isomeke ifuatavyo: “(1) (b) Anajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.”
 
Aidha Dk. Kafumu aliongeza kuwa katika Ibara ya 129 kuhusu haki ya wapiga kura kumwajibisha Mbunge.
 
“Wajumbe wengi wamependekeza kuwa, wapiga kura watumie haki yao ya kumwajibisha mbunge kwa njia ya kidemokrasia ya kupiga kura kila baada ya kipindi cha miaka mitano kinapokwisha. Kamati imeona kuwa, kwa kadri demokrasia ya vyama vingi inayoendelea kukua, upo uwezekano wa watu wachache kuweza kutumia mbinu hasi kumuondoa mbunge anayefaa bila ya kuwa na sababu za msingi. Hivyo basi wajumbe walio wengi wamependekeza ibara hii ifutwe yote.
 
Wakati kwa upande wa maoni ya walio wachache, ambayo yalisomwa na Dk. Tulia Ackson, ambapo alisema katika Ibara 124 inayohusu uchaguzi wa wabunge, walitofautiana na walio wengi kwa kusema kuwa inajitosheleza.
 
“Hii Ibara ni muhimu ibaki kama ilivyo kwani inapunguza matumizi makubwa ya fedha ambayo yameshuhudiwa na wananchi,” alisema Dk. Tulia.
 
Aliongeza kwamba katika Ibara ya 129 walitofautiana na wajumbe wali wengi kwa kusema kuwa ibara hiyo inajitosheleza kwani iwapa wananchi haki ya kuweza kumwajibisha mbunge ambaye hawajibiki ipasavyo katika kuwawakilisha wananchi na kuwatafuatia wananchi ufumbuzi wa matatizo yao. Wajumbe walio wachache walipendekeza ibara hiyo ibaki isipokuwa irekebishwe kama ifuatavyo:
 
129 (1) Bila kuathiri masharti ya Katiba hii, wananchiwatakuwa na haki ya kumwondoa Mbunge wao madarakani, endapo Mbunge atashindwa kuwasilisha aua kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake. (2) Bunge litatunga sheria kuweka masharti ya kuendesha uchunguzi kwa mbunge atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa wapiga kura wake na utaratibu wa kumwondoa katika Ubunge.