Frank Mvungi, Maelezo
SERIKALI imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000 kwa ajili ya makazi ya wanajeshi kote nchini. Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Meja Josephat Musira wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea eneo la Gongo la mboto jijini Dar es Salaam ambapo sehemu ya mradi huo inatekelezwa.
“Lengo la ujenzi wa nyumba hizi ni kupunguza tatizo la muda mrefu la uhaba wa nyumba kwa ajili ya makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa,” alisema Meja Musira.
Akifafanua Meja Musira amesema awamu ya kwanza ya mradi huo imeanza ambapo nyumba 6,064 zitajengwa na kugharimu dola za marekani milioni 300, utekelezaji wake unaendelea vizuri katika Mkoa wa Dar es salaam na Pwani tayari jumla ya nyumba 3128 zinajengwa.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam Meja Musira amesema nyumba 2,228 zinajengwa katika maeneo ya Lugalo, Gongola mboto, Ukonga, Navy Kigamboni, Ubungo Kibangu, Kunduchi KTC, Mbweni JKT na Kimbiji. Akieleza zaidi Meja Musira amesema nyumba 1,160 kwenye maeneo manne ya Lugalo na Gongolamboto umeshakamilika kwa asilimia 100 na ukaguzi na uhakiki umeshafanyika.
Kwa upande wa Mkoa wa Pwani Meja Musira alisema jumla ya nyumba 840 zinajengwa katika maeneo ya msangani, Nyumbu, Kiluvya, Kisarawe na shule ya mafunzo ya awali Kihangaiko. Maeneo yanayohusika na mradi huu kwa sasa ni Arusha inatarajiwa kujengwa nyumba (792) Tanga (312) Pemba (320) Morogoro (616) Dodoma (592) Kagera (144) na Kigoma (160).
Kwa upande wake Mhandisi wa Wizara hiyo, Stephen Mpapasingo amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu na unalenga kuondoa kabisa tataizo la makazi kwa Maofisa na askari wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa. Mkandarasi wa mradi huu ni kampuni ya Shaghai Construction (Group) General Company kutoka China.