Sera Mbaya Ndizo Zinazoulea, Kukuza Ugaidi – Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema moja ya vyanzo vikubwa vya kuzalisha, kulea na kukuza ugaidi duniani ni sera mbaya za ubaguzi na zinazowanyima haki za msingi baadhi ya wanajamii ama makundi ya wanajamii.

Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa ni muhimu kwa mataifa mbali mbali duniani kubuni na kutunga sera ambazo zinalenga kutoa nafasi na haki za msingi kwa kila mwanajamii na mwananchi kufurahia sehemu ya keki ya taifa.

Rais kikwete pia amesema kuwa kwa jumla sera za kichumi na kijamii zina mchango mkubwa katika kukabiliana na kupambana dhidi ya ugaidi na vitendo vya msimamo mkali wenye kutumia nguvu na fujo katika nchi yoyote.

Rais Kikwete aliyasema hayo Septemba 2, 2014 wakati alipozungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta mjini Nairobi, Kenya chini ya uenyekiti wa Rais Idrisa Debby wa Chad.

Katika mchango wake kwenye Mkutano huo, Rais Kikwete alisema kuwa ni dhahiri kuwa ugaidi ni tishio la kweli kweli la Bara la Afrika kwa mujibu wa Ripoti iliyowasilishwa kwenye Mkutano huo na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambayo ilielezea kwa uwazi kabisa tishio la ugaidi.

“Kwa kuongozwa na Ripoti hii, tunatambua sasa kuwa ugaidi ni tatizo gumu sana kwa sababu hakuna nchi duniani isiyoguswa nao na hakuna nchi hata moja duniani yenye uwezo wa kukabiliana nao peke yake. Hivyo, ni muhimu kuunganisha juhudi zetu kwenye ngazi zote: ngazi ya kitaifa, kikanda, kibara na duniani ili kuweza kukabiliana nao ipasavyo,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kuna maswali mawili muhimu ambayo tunastahili kujiuliza na kuweza kupata majibu mwafaka juu ya kwa nini kuna balaa la ugaidi na jinsi gani tunavyoweza kukabiliana nalo. Katika jitihada zaidi za kukabiliana na tatizo hili ni lazima tutafute kiini hasa cha kujaribu kumaliza ugaidi na vitendo vya msimamo mkali wa kutumia nguvu na fujo. Katika hali hii, sera za kiuchumi na kijamii katika kila nchi zina mchango mkubwa katika mapambano haya,” alisema Rais Kikwete.

Alisisitiza: “Mataifa ni lazima yabuni na kutunga sera zenye maslahi kwa watu, sera ambazo zinalenga kuleta maendeleo na ustawi kwa watu wote, sera ambazo hazimbagui yoyote kwa sababu ya kabila lake, dini yake, ama wilaya ama mkoa atokako. Ni lazima tuwe na sera ambazo kila mwananchi ana haki ya kupata huduma za msingi za kijamii na kichumi na kupata mgawo wao wa haki katika keki ya taifa.”

Aliongeza Rais Kikwete: “Ni muhimu kubuni na kutunga sera zinazotoa uhuru na haki za msingi kwa watu wote bila kujali mielekeo na misimamo yao ya kisiasa. Ni pale ambako baadhi ya watu wanajiona wanabaguliwa ama kundi la watu ndani ya jamii linanufaika kupita kiasi na rasilimali za mataifa ndiko yanapojengeka mazingira ya kuzuka na kukua kwa ugaidi.”

Rais Kikwete, hata hivyo, amesema kuwa wakati mwingine ugaidi unaweza usiwe na mazingira ya kuzaliwa ndani ya nchi kama tulivyoona wakati Balozi za Marekani mjini Dar es Salaam na Nairobi zilipolipuliwa kwa mabomu. “Kikundi cha Al-Qaeda kilikuwa na matatizo na Marekani na kikaamua kuzifanya Tanzania na Kenya uwanja wa mapambano.”