*Mlezi wao bibi miaka 80 aomba asaidiwe kisheria
Na Yohane Gervas, Rombo
WATOTO wawili wa Kijiji cha Aleni Chini, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, mmoja akiwa na umri wa miaka 9 na mwingine miaka 6 wote wanafunzi Shule ya Msingi Aleni (majina tunayo) wanadaiwa kulawitiwa na mtu mmoja mkazi wa kijiji hicho.
Akizungumzia Tukio hilo Mkuu wa Shule ya Msingi Aleni, Basley Mkanda alisema tukio hilo limetokea Agosti 21, 2014 ambapo siku ya tukio mmoja wa watoto hao ambaye ni mwanafunzi wa chekechea alionekana akiwa anakaa kwa shida ndipo alipomfuata na kumuuliza na kuanza kusimulia kisa hicho.
“Nilimuuliza kwa nini hataki kukaa akasema ana maumivu sehemu za siri (makalio) nilipompeleleza zaidi akasimulia kisa chote kwamba alikua ametumwa dukani akaitwa na kijana mmoja akampeleka jikoni akaanza kumfanyia kitendo hicho cha kusikitisha,” alisema Mkanda.
Aidha aliongeza kuwa baada ya taarifa hiyo alimwita kaka yake ambaye anasoma darasa la kwanza ili akamwite mlezi wao lakini baada ya kumwita alishangazwa baada na kaka mtu kueleza kuwa alifanyia kitendo hicho pia.
“Alipoenda kumwita kaka yake naye akaeleza kuwa aliwafanyia wote wawili, kweli nilishangaa sana sikuamini,” alisema Mkanda.
Naye kwa upande wake mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho mwenye umri wa miaka tisa akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema kuwa siku ya tukio alikua ametumwa dukani na mlezi wake na ndipo mtuhumiwa alimwita na kumfanyia kitendo hicho
“…Aliniita nilikua naenda dukani…akanivuta akatupeleka jikoni kwake akatuambia tusipige kelele akaanza kutuvua nguo na kutupaka mafuta sehemu za siri kisha akatufanyia hicho kitendo,” alisema mtoto huyo kwa masikitiko.
Alisema kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho kwa mara ya kwanza hakutoa taarifa sehemu yoyote lakini kesho yake alitoa taarifa kwa mwalimu wake.
Naye kwa upande wake mlezi wa watoto hao ambao ni bibi anayekadiwa kuwa na umri wa miaka 80 alisema kuwa amesikitisikitishwa na kitendo hicho.
“Mwandishi naomba mnisaidie hao watoto sijui baba yao wala mama yao niliachiwa wakiwa wadogo ndio nawalea hiki kitendo kweli kimenisikitisha mno siamini naomba serikali inisaidie,” alishindwa kujizuia na kutoa machozi.
Aidha Mashuhuda wa Tukio hilo, John Shirima na Aniset Shao wamelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha aliyejihusisha na tukio hilo anachukuliwa hatua za kisheria kwani ni kitendo kibaya mno walichofanyiwa watoto hao.
Taarifa zaidi ambazo hazijathibitishwa na Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa Polisi. Kamanda wa Polisi Mkoani hapa alipotafutwa ili kuzungumzia tukio hilo hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.