Na Genofeva Matemu – WHVUM
VIJANA kutoka nchi za Afrika ya Mashariki wameshauriwa kujikita katika sekta ya sanaa kwani ni fani ambayo inatoa nafasi kubwa ya ajira kwa vijana hivyo kuondokana na tatizo la ajira katika nchi za Afrika Mashariki.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara wakati wa ziara ya Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) walipotembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) hivi karibuni katika Wilaya ya Bagamoyo.
Dk. Mukangara amesema kuwa TaSUBa ni kituo cha Maarifa kinachotoa masomo ya sanaa za maonyesho yaani ngoma za jadi na michezo ya kuigiza na sanaa ya ufundi wa uchoraji na ufinyangaji Afrika ya Mashariki hivyo ni vyema kwa vijana kujiunga na chuo hicho ili waweze kupata taaluma na kuweza kujiajiri wenyewe.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Spika wa Bunge la EALA Bi. Magreth Zziwa amesema kuwa masuala ya Sanaa na Utamaduni ni muhimu sana katika jamii zetu kwani Utamaduni hujenga umoja, utambulisha jamii husika na kuthamini utajiri wa mila na desturi za waafrika.
Zziwa amesema kuwa Bunge la Afrika Mashariki limejumuisha vituo mbalimbali vya Maarifa vyenye weledi Afrika ya Mashariki na katika vituo hivyo TaSUBa ni moja ya kituo cha Maarifa chenye rasilimali watu, wingi wa ubunifu na mitaala iliyopangika kwani sifa mojawapo ya kituo cha Maarifa kuwa na weledi ilikua ni kituo kuwa na mpango mkakati ambapo TaSUBa wanao.
Aidha Zziwa ameitaka TaSUBa kupenya nchi zote za Afrika ya Mashariki na kuwa na brandi ya Kiswahili kitakachotumika Afrika ya Mashariki pamoja na brandi ya kiutamaduni na kisanaa itakayohusisha nchi hizo kwa kutangaza shughuli mbalimbali za kiutamaduni vikiwemo vyakula vya Afrika ya Mashariki, mavazi na aina ya muziki wetu.
Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TaSUBa, Bw. Michael Kadinde alisema kuwa TaSUBa imeandaa mitaala mipya mbalimbali kwa sasa itakayotumika kwa ajili ya wanafunzi watakao jiunga na Taasisi hiyo kutoka Afrika ya Mashariki.
Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambayo ilianzishwa kwa sharia ya wakala wa serikali Na. 30 ya mwaka 1997 inayotoa mafunzo, utafiti na ushauri katika masuala ya Sanaa na Utamaduni nchini.