Taarifa ya utafiti juu ya matatizo yanayowakabili Wanafunzi wenye ulemavu, hasa wasioona katika baadhi ya shule za msingi Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Lushoto, Tanga.
Mwandishi: Joachim Mushi,
wa gazeti la KULIKONI,
Simu namba: 0717 030 066
au 0786 030 066,
Barua pepe: jomushi79@yahoo.com
Kuanzia Juni 15 hadi Julai 21, 2009.
Yaliomo:
-Sehemu ya kwanza
Hali halisi ya eneo la utafiti kimazingira na jinsi utafiti ulivyofanyika
-Sehemu ya Pili
Taarifa ya utafiti
-Sehemu ya Tatu
Wananchi waliyohojiwa katika utafiti
-Sehemu ya Nne
Taarifa za ziada kwenye utafiti
-Sehemu ya Tano
Hitimisho
-Sehemu ya Sita
Mapendekezo ya mtafiti
Hali halisi ya eneo la utafiti kimazingira na utafiti ulivyofanyika
Wilaya ya Lushoto ni kati ya Wilaya saba za Mkoa wa Tanga nchini Tanzania . Wilaya hii inakadiriwa kuwa na takriban zaidi ya wakazi 419,970 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002.
Hata hivyo, Wilaya ya Lushoto ni sehemu ya milima ya Usambara. Inapakana na Wilaya ya Muheza na nchi ya Kenya upande wa kaskazini, wakati Mashariki – Kusini imepakana na Wilaya ya Korogwe.
Upande wa Magharibi imepakana na Wilaya ya Korogwe pia na Mkoa wa Kilimanjaro.
Wenyeji wa asilia ni Wasambaa na Wambugu. Wilaya imegawanyika katika tarafa nane ambazo ni Lushoto yenyewe, Soni, Bukuli, Mgwashi, Mlola, Mlalo, Mtae na Umba.
Utafiti ulifanyika katika kwa njia mbalimbali kulingana na mazingira ili kupata taarifa kadri zilivyokuwa zikihitajika. Utafiti ulianza kufanyika kwa kufanya mahojiano na baadhi ya makundi muhimu katika kupata taarifa hitajika.
Miongoni mwa makundi hayo ni walimu kutoka shule za walemavu, wananchi, viongozi wa mitaa, viongozi wa Serikali Wilayani hapo na wazazi wa watoto walemavu. Makundi mengine ni pamoja na viongozi wa dini na wadau wa masuala ya utoaji huduma za jamii kwa jumla.
Utafiti umefanyika kwa mahojiano ya mmoja mmoja makundi na uchunguzi pale ilipobidi kulingana na mazingira husika. Utafiti umefanyika mjini Lushoto na nje kwa baadhi ya tarafa.
Taarifa Kamili:
Taarifa kamili inaonesha kunatofauti kati ya ukubwa wa tatizo la wanafunzi wenye ulemavu kutopata huduma stahili na hata haki ya kikatiba inayomtaka kila raia kuwa huru kupata elimu.
Utafiti unaonyesha namna ilivyo kwa baadhi ya shule za Mkoa wa Dar es Salaam ni tofauti katika Wilaya ya Lushoto. Kwa Lushoto tatizo la wanafuzi kutopata haku ya elimu ni kubwa zaidi ukilinganisha na Dar es Salaam .
Kati ya Wilaya yote ya Lushoto kuna shule moja tu ambayo ndio inayopokea wanafunzi wasioona yaani kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba. Shule hiyo inajulikana kwa jina la ‘shule ya Wasioona Irente.
Shule hii ipo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambapo serikali imeingia ubia na kusaidia uendeshaji wa shughuli zake. Shule hiyo iliyoanzishwa miaka ya 1963 ina uwezo wa kupokea wanafunzi 70 tu, ambapo inapokea kutoka mikoa mbalimbali.
Uwezo wa shule ni mdogo na kuna wanafuzi wamekuwa wakirudishwa nyumbani kila unapofika kipindi cha usajili wanafunzi baada ya kukosa nafasi katika shule hiyo.
Shule hiyo ambayo ni ya kulala ipo nje ya mji kiasi kwamba wanafunzi wa maeneo ya mbali na eneo la shule hushindwa kuletwa na kurudishwa baada ya masomo, achilia mbali gharama ambazo baadhi ya wazazi wenye moyo wangeliweza kufanya hizo kwa watoto wao.
Hata hivyo shule inakabiliwa na uhaba wa walimu zaidi ya vitendea kazi hivyo kuwa ni kikwazo kingine cha kushindwa hata kupokea watoto wa kutwa endapo wangeliweza kuletwa shuleni.
Idadi kubwa ya wananchi waliotoa mawazo katika maadalizi ya utafiti huu hawaridhishwi na namna serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto inavyoshughulikia elimu maalumu katika eneo hilo . Wengi wanasema hakuna utaratibu wowote unaofanywa na viongozi wawe wa elimu au halmashauri kuangalia namna ya kuwatambua wanafunzi wasioona na kupatiwa elimu.
Wilaya zima yenye zaidi ya wakazi 400,000 ina shule ya walemavu moja tu tena ya wasioona huku ikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 70 licha ya kutegemewa pia na mikoa mingine.
Mfano mzuri kitengo cha huduma za jamii, KKKT kimelazimika kuzunguka katika baadhi ya vijiji eneo hilo na kupata takriban watoto wenye ulemavu 400 ambao wanahitaji msaada wa elimu lakini wameshindwa kutokana na kutokuwa na shule jirani.
Kitengo hicho kimeanza kufanya utaratibu kwa kushirikiana na wananchi na kuanzisha vituo ambavyo si rasmi vya kutoa elimu kwa watoto wenye ulemavu katika maeneo jirani na vijiji vyao.
Halmashauri hailitambui hilo licha ya kuwa na shule za msingi katika baadhi ya maeneo yalio jirani na wananchi katika vijiji kadhaa. Shule zote za msingi hakuna hata moja yenye kituo cha watoto wenye ulemavu hata cha kutwa mchanganyiko.
Walimu waliohojiwa wanaweka wazi kuwa wilaya nzima hutoa walimu 10 pekee kila mwaka kwaajili ya kwenda vyuoni kupata angalau taaluma ya kufundisha elimu maalumu kiwango ambacho ni kidogo ukilinganisha na mahitaji.
Licha ya muitikio mdogo wa halmashauri juu ya kuwasaidia wanafusi wasioona kupata elimu, kwa kuwa wao ndio wanaowajibika kuwalipa walimu katika shule ya Irente wamekuwa wakiwakataa walimu wenye taaluma ya elimu maalumu kwa madai hawana fedha kwenye bajeti.
Mfano mwaka jana 2008 walimkataa mwalimu aliyeletwa kutoka wizarani kuja kuwasaidia upungufu wa walimu kwa madai hawana fedha na kumrudisha mwalimu huyo alikotoka, huku wakiwa na upungufu wa walimu wa elimu maalumu.
Kimsingi halmashauri ambayo ni wawakilishi wa serikali hawana taarifa zozote za wanafunzi wenye ulemavu, hasa wasioona hata katika shule pekee ya Irente ambayo nao wanachangia uendeshaji. Kibaya zaidi kila viongozi wa shule hiyo wanapojaribu kuhoji wanatishiwa kuondolewa madarakani na uongozi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Wilaya kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri.
Hali ya usambazaji wa vifaa vya kufundishia katika shule hiyo ni wakawaida kutokana na Kanisa kujitahidi kuomba misaada kutoka kwa wafadhili na nguvu za waumini ambao nao wamekuwa wakijitahidi kuleta vifaa.
Kanisa limelazimika kuanzisha kituo kingine kingine kama shule ambacho kitawasaidia wanafunzi wenye mtindio wa ubongo kundi ambalo lilikuwa limesahaulika eneo hilo . Kituo ambacho kwa sasa kinaelekea kukamilika kinajulikana kama ‘Irente Rainbow’ ambacho kipo jirani na shule ya wasioona ya Irente.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam hali ni mbaya zaidi. Mkoa una shule ya wasioona moja tu ambayo ni mchanganyiko na wanafunzi wengine inayojulikana kama Uhuru Mchanganyiko. Wanafunzi wasioona hujifunza hadi darasa la saba na baada ya hapo huchanganywa na wanafunzi wa kawaida na kuanza kufundishwa kwa pamoja.
Hali hii huwaathiri katika mapokeo ya elimu licha ya kukabiliwa na tatizo kubwa la vifaa vya kujifunzia zikiwemo mashine za kuandikia ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.
Shule ina uwezo wa kuchukua wasioona 80 tu na mara zote hulazimika kuwaacha wanafunzi katika usajili kutokana na kukosa nafasi za kuwahifadhi mfumo wa kulala shuleni. Hata hivyo, licha ya mkoa kama Dar es Salaam kuwa na kiwanda cha kuchapisha vitabu vya wasioona lakini bado hata baadhi ya maeneo yanakabiliwa na upungufu wa bidhaa hiyo.
Mbali na hayo vifaa kama mashine za kuandikia kwa wanafunzi wasioona kwa shule kama ya Uhuru Mchakanganyiko iliyopo Ilala Dar es Salaam nitatizo kubwa. Upungufu wa walimu pamoja na ufinyu wa nafasi za wasioona kujiunga na shule. Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Uhuru Mchanganyiko anasema kila mwaka hulazimika kuwaacha baadhi ya wanafunzi wasioona baada ya nafasi kujaa shule hiyo.
Hata hivyo wanafunzi wasioona wanakabiliwa na upungufu pia wa walimu wa kufundisha elimu maalumu, hali hii husababisha walemavu hawa kuchanganywa na wanafunzi wa kawaida na kufundishwa pamoja. Mfano halisi ni shule ya Uhuru Mchanganyiko Dar es Salaam ambayo huwachanganya pamoja. Mwanzoni wanafunzi wasioona husoma toka darasa la kwanza hadi la tatu na baada ya hapo huchanganywa na kujifunza pamoja.
Hali hii ni tatizo kwani imeendelea kuzorotesha elimu ya walemavu wasioona kwa kutopata muda na nafasi ya kutosha kueleweshwa na kupata ufafanuzi kutoka kwa mwalimu.
Mara nyingine walimu huwa wakiwafundisha kama wanafunzi wa kawaida kutokana na darasa kuwa na wanafunzi wa kawaida wengi kupita wale walemavu.
Chanzo cha tatizo;
Kimsingi matatizo katika utafiti huu, yanatofautiana kutoka eneo moja hadi lingine kati ya maeneo yote yaliofanyika utafiti huu; yaani kwa baadhi ya shule za Mkoa wa Dar es Salaam na wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga. Hali hii ni kutokana na mwamko wa viongozi na hata utayari wa wananchi kuchangia kwa namna moja ama nyingine suala zima la kuinua elimu kwa wasioona.
Kwa Wilaya ya Lushoto tatizo lipo kwa viongozi wenyewe wa halmashauri ya wilaya hiyo. Viongozi hao hawana utaratibu wowote hata katika hali ya kawaida wa kutengeneza ama kuandaa mazingira ya elimu kwa walemavu hasa wasioona.
Licha ya taasisi kama za dini kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya walemavu hao kupata elimu mwamko kwa viongozi bado ni mdogo. Kwa mfano viongozi wa halmashauri kitengo cha elimu umekuwa hata hauna taarifa za muhimu katika shule moja tu iliyopo katika eneo hilo ‘Irente’.
Mwamko mdogo wa viongozi hili limeonekana wazi kwani hata katika shule za walemavu zinazoanzishwa na taasisi za dini serikali imekuwa ikitoa ushirikiano kwa kusita sita.
Mfano KKKT- Lushoto wameanzisha shule nyingine ya watoto wenye mtindio wa ubongo lakini hadi muda huu, serikali ya wilaya bado haijaongeza nguvu zinazostahili kutokana na umuhimu wa kituo hicho.
Pia wamediriki kuwarudisha walimu wenye elimu maalumu mara kadhaa katika wilaya hiyo licha ya shule zao kukabiliwa na uhaba wa walimu wa aina hiyo.
Pia eneo la Lushoto viongozi wanashindwa kupangilia vizuri bajeti ya sekta husika inayotumwa kutoka serikali kuu, hivyo kushindwa kuweka utaratibu wa kuwasaidia kielimu wanafunzi walemavu wasioona kutoka katika familia zao.
Zipo baadhi ya juhudi ambazo zingeliweza kuchangia uboreshaji wa huduma kwa walemavu hasa katika kuchapisha vitabu vya wasioona baada ya serikali mwaka juzi kununua mtambo wa kuchapisha vitabu vyao.
Kibaya mtambo umeshindwa kwenda na kasi ya uchapishaji vitabu kutokana na kila shule kuwa na uamuzi wa kutumia kitabu chochote kwaajili ya kufundishia.
Hali hiyo imefanya kila shule kuwa na vitabu vyake, kabla ya kiwanda kushindwa kichapishe kitabu gani. Taarifa na uhamasishaji unaofanywa na kitengo cha elimu maalumu chini ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi hazitolewi ipasavyo hivyo hata jamii kukosa mwamko.
Bado shule za walemavu zinapata shida namna ya kufuatilia vifaa na nyenzo nyingine makao makuu ya Dar es Salaam hali inayoleta shida kwa shule husika. Utaratibu huo bado unaendelea hadi leo kitendo kimechocangia kwa namna moja ama nyingine ugumu wa utoaji elimu kwa kundi hilo .
Watu waliohojiwa:
Watu waliohojiwa na anwani zao/namba za simu ni kama ifuatavyo:-
1) Sophia Mjema- Mkuu wa Wilaya ya Lushoto-
2) Celina Magambo- Mkuu wa shule ya Wasioona Irente- 0782359287
3) Mshahura Ruben- Ofisa Utawala shule Irete -0787901342
4) Sezaria Kiwango- Mwl. Mkuu Msaidizi s/m Uhuru Mchanganyiko- 0756050228.
5) Joyce Kibanga Mkurungezi Huduma za Jamii- KKKT, Lushoto. 0784350264
6) Prof. Jumanne Maghembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi- 0786034888
7) Elius Nasamaki- Katibu wa Chama Cha Walemavu Tanzania-
8) Mwantumu Mahiza, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi- 0754372918
9) Magreth Kishiwa-Meneja kiwanda cha vitabu cha wasioona-0784811971
10) Shida Salum-Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania- 0713472061
11) Mr. Kishiwa- Ofisa Uhusiano Wizara ya Elimu- 0222120412
12) Salum Mwaya -Mwalimu-Lushoto.
13) Jonathan Mhina-Ofisa Elimu wa Wilaya Lushoto.
14) Lyaku Willy- Mkazi wa Dar es Salaam mda wa haki za jamii ya walemavu.
15) Ofisa Tawala Wilaya ya Lushoto- 0754023504
16) Lucy Msoffe- Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Lushoto-
17) P. Mushi- Ofisa Elimu Msaidizi Wilaya ya Lushoto-
18) Mzee Kiungulila- Mkazi wa Soni.
19) Henry Edward – Mkazi wa Soni.
20) Kakaa Mwashembelwa- Mkazi wa Mlola.
21) Dk. Sam Jowele- Bukuli- Mkazi wa Lushoto.
22) Merry Mtimbi Mkazi wa kijiji cha Irente.
23) Bahia Abubakar Mkazi – Buguruni Dar es Salaam.
24) Adrian Abdallah Mkazi Mlola- Lushoto.
25) Mwanaidi Said Mwanafunzi- Soni.
26) Kasim Rashid Mkazi wa Sanya- Mlola-Lushoto.
27) Kulwa Tapa Mkazi wa Irente.
28) Juma Milanzi Mkazi wa Lushoto view Point.
29) Shaban Kilumbe- Mkazi wa Dar es Salaam- 0754622665.
30) Mwanaidi Mketo- Mkazi wa Dar es Salaam .
31) Athuman Chihua Mkazi wa Lushoto mjini.
Taarifa ambazo hazikuripotiwa kwenye makala:
Hata hivyo, zipo baadhi ya taarifa hazikuweza kuripotiwa katika mfululizo wa makala na habari zilizotoka katika utafiti mzima. Taarifa hizo ni pamoja na mgogoro uliopo kati ya shule ya wasioona ya Irente na uongozi mzima wa Wilaya ya Lushoto.
Licha ya shule hiyo kumilikiwa kwa ubia na Serikali kumekuwa hakuna ushirikiana mzuri kati ya uongozi wa shule na Halmashauri kwa madai viongozi wa shule wamekuwa wakitoa siri za serikali na kutupa lawama za kutelekezwa.
Kwa kifupi mwalimu mkuu wa shule ya Wasioona Irente ameshawahi kutishiwa kuondolewa nyazifa aliyonayo sasa endapo ataendelea kuilalamikia serikali juu ya mapungufu yoyote katika shule hiyo.
Uongozi wa elimu wilaya hiyo umekuwa ukimtishia kutoongea na chombo chochote cha habari juu ya mapungufu yaliopo katika shule yake kwani kufanya hivyo ni kuidhalilisha serikali.
Zipo taarifa ambazo hazikuingizwa katika makala mbalimbali za uchunguzi wa utafiti huu, lakini nazo zimejitokeza na kuoneka ni chanzo cha kuzolota kwa shughuli nzima. Mwalimu huyo amekuwa akipigwa marufuku kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa madai amekuwa akiuchongea uongozi wa halmashauri kwa kutoijali shule hiyo.
Utafiti umebaini kuwa kutokana na uongozi wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kuwa mbali na maendeleo ya shule hiyo, uongozi hauna taarifa zozote sahihi za shule licha ya serikali kuwa mbia katika uendeshaji.
Mkuu wa wilaya hajawahi kuitembelea shule hiyo tangu ameingia madarakani miaka miwili iliyopita; zaidi ya kwenda shuleni pale anapokuwa amealikwa katika sherehe za mahafali ya wanafunzi.
Ushahidi halisi, Ofisa Elimu Msaidizi wa Wilaya ya Lushoto alishindwa kutoa taarifa sahihi za walemavu waliopo katika shule ya Irente hali ambayo inathibitisha kweli kuna hali ya kutokuwa makini juu ya elimu kwa walemavu.
Hata hivyo, katika mahojiano Ofisa Elimu Msaidizi wa Wilaya ya Lushoto alishindwa kueleza namna ambavyo halmashauri kupitia kitengo cha elimu imevyokuwa ikifanya taratibu mbalimbali za kushughulikia suala zima ya elimu kwa walemavu.
Mkurugenzi Mtendaji, akifanya mahojiano na utafiti huu alikiri mwaka jana halmashauri iliwarudisha walimu wa elimu maalumu ambao waliletwa kuja kufundisha katika shule ya Irente kwa madai wilaya haikuwa na fungu la kuwalipa kutokana na ufinyu wa bajeti. Hata hivyo, hali hiyo ilifanyika huku kituo kikikabiliwa na upungufu wa walimu.
Hitimisho:
Ni wazi kuwa hali ya vifaa kuanzia vya kufundishia, vitabu vya kujifunzia na nyenzo nyingine kwa walemavu hasa wasioona ni mbaya zaidi.
Yapo maeneo ambayo licha ya kuwa na upungufu wa vifaa wamekuwa hawana majengo kabisa ya shule maalumu licha ya baadhi ya wazazi kuwa na mwamko. Katika hali hiyo serikali ina kila sababu ya kuanzisha msukumo wa nguvu kunyanyua elimu kwa walemavu ili kuwakomboa.
Walemavu wanaweza kujitegemea endapo watapata elimu ya kutosha na na msingi mzuri wa kuandaliwa kimaisha. Mfano mzuri ni namna shule ya Irente ilivyotoa walemavu ambao kwa sasa wanajitegemea kimaisha; licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kwa taifa pia. Walemavu hawata kuwa mzigo endapo watapewa urithi wa elimu inayofaa na kujengwa mapema kisaikolojia.
Mapendekezo:
Serikali ina kila sabanu ya kusaidia kuinua mchakato wa elimu maalumu kwa walemavu ili kujiondolea mzigo wa watu hao kuitegemea kwa mambo kadhaa.
Viwanda vinavyochapisha vitabu na vifaa vingine kwa walemavu visambazwe katika shule zote husika ili kupunguzia gharama za mizigo kwa shule husika katika maeneo mbalimbali.
Licha ya kupoteza gharama kumekuwa na safari zisizokuwa na matiki huku zikipunguza ufanisi wa wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yao . Ipo haja ya kiwanda cha kuchapisha vitabu vya wasioona kuanza kuchapisha vitabu vya wanafunzi wenye uoni hafifu ili nao waweze kutumia vipaji vyao jijini Dar es Salaam.
Serikali ibadili utaratibu na kuzilazimisha shule kutumia kitabu cha aina moja kwa darasa moja kulingana na kidato cha mwanafunzi, ili kurahishisha kiwanda kufanya kazi ya kuandaa na kuhifadhi vitabu vya wasioona.
Kiwanda kimeshindwa kuchapa vitabu na kuhifadhi kutokana na kila shule kuwa na kitabu chake tofauti kwa kila darasa.
Mwisho serikali ina kila sababu kujitahidi kutoa kiasi cha shilingi 20,000 kwa kila mlemavu zipelekwe katika shule ili kusaidia gharama za elimu kwa wanafunzi. Kwani hadi leo licha ya utoaji wa elimu kwa walemavu kuwa mgumu kutokana na ughali wa vifaa na mazingira bado serikali imekuwa ikitoa kiwango kimoja kwa wanafunzi wote wastani wa shilingi 10,000 kwa kama gharama ya elimu.
Mwisho