Na Gelvas Yohane
MADIWANI wa Wilaya Rombo mkoani Kilimanjaro wamemtaka Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Maje kutoa ufafanuzi juu ya fedha zaidi ya shilingi milioni 46 zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa kiwanda cha maziwa na ufugaji wa samaki.
Wakizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wametaka kupewa taarifa kwanini tangu fedha hizo kutengwa mwaka 2006 hakuna kinachoendelea. Diwani wa Kata ya Mrao Keryo, Flavian Marandu, alisema fedha hizo sh. 46 zilitolewa muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo lakini mpaka sasa haijakamilika, ilhali fedha zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji.
Diwani Marandu alisema kutokamilika kwa miradi hiyo kumezua hofu kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo, hivyo wanataka kufahamu ni kwa nini mradi huo haujakamiliki huku Serikali tayari imeshatenga fedha. Kutokana na malumbano hayo Mwenyekiti wa Baraza hilo, Antony Tesha, alimtaka Mkurugenzi, kupeleka wakaguzi kukagua miradi hiyo ili kubaini tatizo la kuchelewa kwa miradi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika baraza lijalo.
“…Miradi hii ilianza kutengewa fedha za utekelezaji toka mwaka 2006 akiwepo Mkuu wa Mkoa, Mohamed Babu, akaingia Monica Mbega, Saidi Kalembo na sasa yupo Leonidas Gama lakini bado miradi hiyo haioneshi dalili za kukamili kweli kunahitaji uchunguzi wa kina,” alisema Tesha.
Alisema wananchi wilayani humo wanashindwa kuinuka kiuchumi kutokana na kutokamilika kwa miradi hiyo, pamoja na kutopewa elimu ya ufugaji wa kisasa.