Na Mwandishi Wetu, Kiteto
“NAPENDA kusoma, na ninataka niwe mwanasheria ili niwaokoe wengine kutokana na migogoro ya ardhi,” anasema Paschal Michael, mtoto wa miaka 10 anayesoma katika shule ya msingi Boma mjini Kibaya. “Elimu ni muhimu sana kwangu, lakini ni muhimu sana kwa Watanzania wote hasa walio maskini, inaweza kuwainua kiuchumi.”
Paschal anakumbuka madhira yaliyompata yeye na familia yake miaka minne iliyopita wakati huo akiwa na miaka saba (7), wakati serikali ilipowahamisha kwa nguvu wakazi wote wa kitongoji cha Laitimi na vitongoji vya Laipera, Laipenu na Tasaf katika Kata ya Partimbo, wilayani Kiteto.
Mtoto huyo wa darasa la nne sasa, ambaye wakati huo, yaani mwaka 2006, alikuwa darasa la pili, alilazimika kusimama masomo kwa mwaka mzima wakati wazazi wake, wakiwa miongoni mwa mamia ya wakazi wa vitongoji hivyo, walipokuwa wakihaha huku na huko kusaka makazi mapya.
“Nakumbuka sana wakati huo mvua ilikuwa inanyesha na mama yangu alikuwa anaumwa sana, lakini baada ya vikosi vya mapolisi kuja wakazi wote wakaamuliwa kuondoka, bila kujali kwamba ulikuwa msimu wa kilimo wala kama kulikuwa na watoto ambao wasiengeweza kutembea umbali mrefu hasa kwa vile hakukuwa na usafiri wowote,” anakumbuka mtoto huyo, ambaye baba yake ni Mchungaji wa Kanisa Anglikana aliyelazimika pia kuhama baada ya kanisa alilokuwa akiliongoza kitongojini hapo nalo kuvunjwa.
Paschal anaendelea kusema kwamba, ingawa yeye alikuwa akisoma katika shule ya msingi Ngeju alikokuwa akiishi kwa wasamaria wema, lakini kitendo cha wazazi wake kuhamishwa kwenye kitongoji hicho kilimaanisha kwamba hata yeye alitakiwa kuungana nao kwena kusikojulikana.
Mtoto huyu alikuwa miongoni mwa watoto wengi wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi 13, ambao walilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 150 kunusuru maisha yao huku polisi wakiwa wamevunja ‘nyumba’ zao za nyasi katika vitongoji hivyo ambavyo ni maarufu kwa shughuli za kilimo.
Wengi wa watoto hao walikuwa ni wanafunzi ambao walilazimika kuacha shule baada ya wazazi wao kukosa makazi na kuhamia maeneo mengine ya mbali ili kuendesha shughuli za kilimo wanazozitegemea kiuchumi. Mateso waliyopata, anakumbuka mtoto huyo, ni kutembea kwa kilometa nyingi kwa miguu, mvua ikiwanyesha wakati mwingine, huku mama yake mzazi anayesumbuliwa na ugonjwa wa pumu akiwa hoi bina taaban.
“Kwa kweli nikikumbuka kipindi kile, japo bado mdogo, machozi hunitoka. Nilidhani mama yangu angekufa kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya sana. Tulitembea nadhani kwa siku nne hadi katika kijiji kingine ambako baba alipangiwa kuongoza kanisa jingine. Bahati nzuri hatukukaa sana, ndipo akahamishiwa huku Kibaya,” anasema kwa uchungu.
Anaongeza: “Nataka nisome sana, na zaidi sheria, ili siku moja nije niwatetee wale wanaonyanyasika kama ilivyokuwa kwetu.” Kisa cha mateso yote hayo ni hatua ya serikali kuchoma nyumba na kuwafukuza kwa nguvu wakazi wa kitongoji cha Laitimi pamoja na vitongoji hivyo vingine vya Laipera, Laipenu na Tasaf katika Kata ya Partimbo kwa madai kwamba wakazi hao walikuwa wamevamia hifadhi ya asili ya Emboley Emurtangos.
Lakini kitongoji cha Laitimi kiliathirika zaidi kutokana na mapigano yaliyokuwa yameibuka awali baina ya wakulima na wafugaji waliokuwa wakigombea ardhi na kusababisha vifo vya watu watatu – mkulima mmoja na wafugaji wawili wa jamii ya Kimaasai.
Mapigano hayo, kwa mujibu wa habari za uchunguzi, yaliifanya serikali kuwafukuza wakulima kwa maelezo kwamba ndio waliokuwa wamevamia maeneo ya wafugaji kinyume cha utaratibu, hususan hifadhi ya asili ya Emboley Emurtangos.
Uchunguzi huo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, ulisababisha watoto zaidi ya 100 wa kitongoji hicho na vingine vya jirani kuyumba kimasomo baada ya shule iliyokuwepo katika kitongoji cha Olkel walikokuwa wanasoma, umbali wa kilometa 15 kutoka Laitimi, kuvunjwa na wanafunzi wote kuhamishwa.
“Wako watoto waliohamishiwa shule ya Lesoit katika kata ya Sunya, wengine wakahamia Namelock katika kata ya Partimbo, lakini walio wengi hawakuendelea na shule kutokana na wazazi wao, ambao walilazimika kuyaacha mazao yao machanga shambani, kuhamia sehemu nyingine kusaka makazi mapya,” anasema Fikiri Mwegoha, mkazi wa kitongoji hicho cha Laitimi.
Aidha, Mchungaji Michael Mahelela, anasema kwamba yeye na familia yake, wakiwemo watoto wao Paschal (10) na Prosper (8) waliokuwa wakisoma shule ya msingi Ngeju, walilazimika kutembea kwa miguu umbali wa kilometa 130 baada ya kufukuzwa katika kitongoji cha Laitimi, hivyo kuwafanya watoto hao wasiweze kuendelea na shule.
“Nilikuwa naongoza kanisa hapo Laitimi, lakini likawa limevunjwa baada ya askari wa kutuliza ghasia (FFU) kuwahamisha kwa nguvu wakazi wote… sikuwa na mahali pengine, ikabidi niondoke na watoto wangu ambapo yule mkubwa aliyekuwa na miaka 7 wakati huo akiwa darasa la pili, alikosa shule kwa mwaka mzima kabla ya kuanza tena kusoma mwaka jana,” anasema Mchungaji Michael, ambaye kwa sasa yuko Kibaya.
Aidha, Mchungaji huyo anasema watoto waliokosa masomo si wale tu waliokuwa wakisoma shule ya Olkel iliyoamriwa kuvunjwa, bali wengine walikuwa wakisoma shule za vijiji vingine kama Nhati, Emalt, Ngeju na kwingineko.
“Mwelekeo wa wazazi wengi ulipotea hasa ikizingatiwa kwamba kipindi hicho kilikuwa cha kilimo na tukaambiwa tuyaache mazao yetu. Isingekuwa rahisi kwa mzazi au mtoto kufikiria suala la shule wakati hata mahali pa kujihifadhi palikuwa shida,” anaongeza.
Wakizungumzia tukio la kuchomewa nyumba zao na kuhamishwa kwa nguvu, wananchi hao wanasema polisi wa FFU wakiwa katika magari matatu walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya watu wenye silaha za jadi waliogoma kuhama.
“Wakati watu wanahangaika na moshi wa mabomu ndipo FFU walipobomoa na kuchoma moto nyumba zetu za nyasi na kuteketeza hata mali zilizokuwemo ndani,” wanaongeza.
Aidha, wanasema waathirika wakubwa wa tukio hilo ni watoto ambao siyo tu walikosa nafasi yao ya msingi ya kwenda shule, bali pia walilazimika kutembea umbali mrefu porini huku mvua kubwa ikiwanyeshea wakati wazazi wao walipokuwa wakisaka makazi mapya.
Ingawa kitongoji hicho bado kingalipo baada ya wananchi kufungua kesi mapema mwaka huu katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi jijini Dar es Salaam kupinga kuhamishwa, lakini watoto wengi wameshindwa kuendelea na shule ama wamerejeshwa katika mikoa wanakotoka wakulima hao, ambao wengi ni wahamiaji.
Diwani wa Kata ya Partimbo, Michael Lepunyati, anakiri kutokea kwa tukio hilo, lakini anasema kitongoji hicho cha Laitimi ni haramu kwani kimejengwa katika mbuga ya hifadhi ya asili, maarufu kama Embley Emurtangos.
Hata hivyo, pamoja na serikali kuwahamisha wakazi hao na kuwatafutia shule nyingine wanafunzi husika, wengi wameacha masomo na kuwa ‘wakulima’ katika umri mdogo baada ya kujikita katika maeneo mengine ya mbali zaidi na zilipo shule pamoja na wazazi wao. Wengine wameingia kwenye biashara na wengine ama wanafikiria kuoa ama kuolewa katika umri mdogo sana.
“Nina miaka miwili tu kuanzia sasa niataka nioe, nijenge mji wangu mwenyewe na kuanzisha familia,” anasema Julius Makapi, 15, siyo jina lake halisi, “Ilikuwa nimalize shule mwaka 2008, lakini baada ya familia yangu kuhamishwa kule Laitimi nami nikaamua kuvua sare na kushika jembe kuandamana nao kusaka maisha.”
Tukio hilo limeendelea kuacha makovu kwa wanajamii, hususan watoto ambao walipata mateso makubwa wakati waliposhuhudia wazazi wao wakinyanyasika mbele ya polisi wa FFU, nyumba na mali zao vikiteketezwa huku wananchi wakishindwa kuokoa kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Utamwelezaje mtoto akakuelewa kwamba wewe baba una nguvu wakati umeshindwa kuokoa hata kibaba cha mahindi wakati polisi walipounguza nyumba yako? Ni jeraha kubwa, ambalo kovu lake litazidi kuonekana miaka nenda rudi hata kwa wazazi wenyewe.