Nyota wa soka Japan Naoki afariki dunia

Marehemu, Naoki Matsuda enzi za uhai wake.

MCHEZAJI Kandanda wa Japan, Naoki Matsuda amefariki dunia siku mbili baada ya kupoteza fahamu uwanjani akiwa mazoezini huku ikiaminika kifo chake kimetokana na maradhi ya moyo.

Matsuda (34), aliyeiwakilisha Japan katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002, alikimbizwa hospitalini siku ya Jumanne baada ya tukio la kuanguka akiwa mazoezini. Alikuwa akifanya mazoezi na klabu yake ya Matsumoto Yamaga, na hakurejewa na fahamu tena hadi kifo chake.

Meneja wa zamani wa timu ya taifa ya Japan, Philippe Troussier akitoa rambirambi zake kwa familia ya mchezaji huyo, alisema alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha nchi hiyo kilichoshiriki Kombe la Dunia.

“Inasikitisha sana kuona mtu anafariki dunia akiwa na umri mdogo kama wake…ni pigo kubwa. Alikuwa kijana mzuri sana na nilikuwa karibu naye. Niko pamoja na jamaa zake katika msiba huu mkubwa,” alisema Troussier.

Mashabiki, marafiki na wachezaji wenzake wa zamani, walikusanyika katika hospitali ya Matsumoto kumtakia apone haraka alipokuwa amepoteza fahamu.

Matsuda aliichezea Japan mara 40 na kushinda mataji mara mbili katika Ligi ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka 15 cha uchezaji wake na timu ya Yokohama F-Marinos. Mapema mwaka huu alijiunga na timu ya Matsumoto inayocheza ligi ya chini.