Na Aron Msigwa – MAELEZO, Kagera
MKOA wa Kagera umechukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa kuongeza udhibiti na ukaguzi wa raia wa kigeni kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoingia nchini Tanzania kupitia vituo vya mpakani vya mkoa huo.
Akizungumza katika mahojiano maalum wilayani Ngara, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe alisema kuwa kufuatia hali hiyo Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeongeza vifaa kinga na kuwawezesha kielimu wataalam wa afya walioko katika hospitali za mkoa huo na vituo vya ukaguzi mpakani.
Alisema mkoa huo kijiografia unapakana na nchi tatu zikiwemo Uganda kwa upande wa Kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi na kuongeza kuwa mkoa kupitia kamati za Afya na wataalam wa afya walioko maeneo yote ya vituo vya ukaguzi wanafanya kazi zao ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa kila anayeingia nchini kupitia vituo hivyo anachunguzwa dalili za Ebola.
“Mkoa wa Kagera kama tunavyojua unapakana kwa karibu sana na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kuna mwingiliano mkubwa sana wa watu kutoka eneo moja kwenda jingine hapa lazima tuchukue tahadhari kubwa , ninawahakikishia wananchi kuwa tumejipanga vizuri katika kuimarisha uchunguzi kupitia kamati zetu za afya,” Amesisitiza.
Amesema kufuatia uwepo wa ugonjwa huo katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uongozi wa mkoa kupitia kamati ya Afya na ile ya Ulinzi na Usalama unaendelea kuwaelimisha wananchi kupitia vituo vya mbalimbali vya radio vya mkoa huo kuhusu dalili za ugonjwa huo, namna ya kujikinga na namna ya kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Kwa upande wake Afisa Afya wa Kituo cha ukaguzi cha Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi, Amos Mangaluke akizungumzia hali ya ukaguzi wa raia wanaoingia nchini kupitia mpaka huo amesema kuwa zoezi la uchunguzi wa dalili za awali za ugonjwa wa Ebola linafanyika kwa ufanisi mkubwa kufuatia kituo chake kuwa na vifaa kinga vinavyomsaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
Alisema takribani watu 500 wanaotumia mpaka huo wa Kabanga huchunguzwa afya zao kwa siku ambapo hujaza fomu maalum ya taarifa ambayo hutumiwa na wataalam wa afya kituoni hapo.