TMA Yawatahadharisha Wakazi Ukanda wa Pwani

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, Dk. Agness Kijazi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, Dk. Agness Kijazi

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wakazi wa ukanda wa Pwani kuchukua tahadhari ya uwezekano wa kuvuma upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa ambayo huenda yakaleta madhara kwa wakazi hao.

Hali hiyo inatarajia kujitokeza kati ya Septemba Mosi, 2014 hadi Septemba 2, 2014. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA kwa vyombo vya habari maeneo ambayo yanatarajiwa kuathiriwa na hali hiyo ni Pwani ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa hali hiyo itasababishwa na kuimarika kwa mgandamizo mkubwa wa hewa
katika maeneo ya kusini mwa Afrika hivyo, kusababisha upepo mkali wa Kusi, Mashariki mwa Pwani ya Tanzania.

“…Upepo mkali unaoambatana na mawimbi makubwa vinatarajiwa katika maeneo yote ya ukanda wa Pwani.
Hali ya Upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2.0 inatarajiwa katika ukanda wote wa Pwani,” ilisema taarifa hiyo.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imewataka wakazi wa maeneo yaliyotajwa kuchukua tahadhari na inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo pale itakapobidi.