WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro wameunga mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba wakisema kuwa wanaridhishwa na hatua iliyofikiwa na mwendo mzima wa Bunge hilo na kuwa mwafaka unawezekana kuhusu vipengele viliyobakia na kupatikana kwa theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya.
Wanafunzi hao wameeleza msimamo wao huo, Agosti 25, 2014, chuoni hapo kwenye risala ambayo wameisoma hadharani mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ametembelea chuo hicho ikiwa sehemu ya ziara yake ya siku saba Mkoani Morogoro.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Bwana Boniface Maige Juma, wanafunzi hao wamesema kuwa ni vyema mchakato huo ukaungwa mkono na kila Mtanzania ili kuuwezesha kuleta neema na matarajio yanayokusudiwa.
Amesema Bwana Juma: “Mheshimiwa Rais, tunaridhishwa sana na hatua iliyofikiwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunaamini kuwa mwafaka unawezekana kwa vipengele vingine vya Rasimu ya Katiba. Aidha, tunaamini kuwa theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya zinawezekana kupatikana.”
Akijibu risala hiyo, Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wanazuoni, watumishi wengine wa chuo hicho na wanavijiji vya jirani na chuo: “Maoni yenu ndiyo maoni yangu. Ni jambo la kusikitisha kuwa tofauti hizi za viongozi wa siasa zinaleta mfarakano wa namna hii. Tokea mwanzo niliwaambia kuwa wakijiruhusu kushindana na kuviziana katika mchakato huo watakwama.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha, niliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa siyo Katiba ya CCM, ama ya CHADEMA, ama ya NCCR, ama ya CUF. Niliwaambia kuwa hii ni Katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubali kwa yale ambayo hatuna tofauti.”
Kuhusu madai kuwa Rais Kikwete anakataa kukutana na wajumbe wa Bunge hilo ambalo wanaendelea kususia shughuli za Bunge hilo, Rais Kikwete amesema: “Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami, ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete ameongeza kuwa ana matumaini kuwa mchakato huu utaweza kuwapatia Watanzania katiba mpya.
“Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli kweli tutafika tuendako vizuri.”